MHESHIMIWA RAIS, TUNAOMBA UTUWEKEE WAJESHI MTAANI

Na, Edward chacha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakula viapo vitatu: Kiapo cha kwanza ni cha utii, ambapo anaapa kuwa atakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wake wote, na kwamba ataihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Kiapo cha pili ni cha Rais, ambapo anaapa kwamba atatenda kazi zake za Urais kwa uaminifu na kutimiza wajibu wa kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu, na kwamba atawatendea haki watu wote kwa mujibu wa Sheria, mila na desturi za Tanzania bila woga, upendeleo, huba wala chuki.

Na Kiapo cha tatu na cha mwisho alacho rais ni cha kudumisha Muungano, ambapo anaapa kwamba ataitetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ingawa katika viapo vyote vitatu rais hatamki waziwazi kuhusu ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao, lakini kiufanisi rais kama amiri jeshi mkuu wa nchi anawajibika kabisa kuhahikisha kuwa usalama wa raia pamoja na mali zao sikuzote unadumishwa;-kwamba, kwa kutumia dhamana aliyokabidhiwa na wanachi,rais anazo nguvu na mamlaka tosha ya kutumia vyombo vya usalama viivyopo kuhakikisha kuwa amani na usalama wa taifa hautiwi hatiani kwa namna moja ama nyingine na wale wabaya wasiolitakia mema taifa letu. Isitoshe sera ya chama tawala ya ulinzi na usalama inatamka waziwazi kwamba vyombo vya usalama vitahakikishia taifa utulivu na amani.

Ndugu amiri jeshi mkuu, matukio ya wizi, ujambazi na uporaji wa kutumia silaha kali na za kisasa unaondelea nchini ni kielelezo kwamba amani Tanzania imeanza kutoweka taratibu. Sijui kama unaliona hilo?

Inasikitisha kuona kuwa pamoja na matukio mengi mabaya ya ujambazi yanayo ambatana na mauaji ya raia wasio na hatia, rais bado anapiga porojo za hapa na pale na kutishia kwa maneno matupu kuwa siku za majambazi sasa zinahesabika huku akiangalia hali hiyo ikizidi kuwa mbaya kila kunapokucha na wala asichukue hatua madhubuti za kutekeleza viapo alivyokula kulitumikia taifa kwa moyo wake wote na kuhakikishia umma usalama wao kama ilivyoelezwa katika ilani ya chama tawala...

Naamini hivi sasa wananchi wana wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya  usalama wa maisha yao   baada  ya jeshi la polisi nchini kushindwa kabisa kukabiliana na majambazi ambayo kwasasa yanaoneka kuwa mbele hatua tatu kimbinu ukilinganisha na jeshi hilo. Toka Kagera hadi Rukwa, wananchi wamejawa hofu tele na wanalala matumbo-joto maana kesho hawajui majambazi hayo yatapora na kuua wapi.

Achilia mbali suala la majambazi hayo kulizidia mbinu jeshi la polisi, kinachokera zaidi ni kwamba wapo baadhi ya askari wachafu ndani ya jeshi la polisi wanaoshirikiana na majambazi hayo kufanya vitendo viovu vya uharifu! Wananchi wanaona mapungufu hayo ambayo viongozi wa serikali akiwemo mkuu wa jeshi la polisi, waziri wa usalama wa raia pamoja na amiri jeshi mkuu ama hawayaoni, au hawana ushupavu wa kuyashughulikia.

Ndugu rais, kama huyo mkuu wa jeshi la polisi pamoja na vijana wake wameshindwa kabisa kukabilia na tatizo la ujambazi nchini, kwanini usitumie jeshi la wananchi wa Tanzania kurudisha nchi katika hali ya utulivu na usalama? Chonde rais, tuwekee wajeshi mtaani...

Pia tunakuomba uwapatie wajeshi hao zana bora zaidi na za kisasa ili kuhakikisha kuwa wanakabiliana na majambazi hayo vilivyo na kulinda usalama wa raia na mali zao ipasavyo. (Majambazi wakija na mashine-guns, wajeshi wapatie RPG-7V). Waongezee mishahara pia ili kuwapandisha mori wa kuyasaka majambazi hayo na kuyakatilia mbali kabisa. Usisahau pia kumfukuza kazi Mahita maana ameshindwa kabisa wajibu wake.

Mh.Kiwete, Waanchi wana matumaini makubwa sana na serikali yako ya awamu ya nne, tafadhali usiwaangushe. Linda usalama wao. Hakikisha kuwa Tanzania inazidi kuwa kisiwa cha amani na utulivu. Watanzania tusingependa kabisa kuona sifa nzuri ya nchi yetu ikitiwa doa na wahuni wachache ndani ya jeshi la polisi.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.