MWAFRIKA, NANI "DADDY" YAKO ?

Na, Magabe Kibiti [Posted:2/3/06]

Ajabu sana!! kila siku utasikia watu Afrika wakipayuka “…Oh vijana wa siku hizi wamepotoka, wanaiga tamaduni za kigeni, wanavaa nguo za ajabu, blaaa..., blaaa...” Kitu kimoja najiuliza, hivi tamaduni asili ya mwafrika ni ipi? Ni nini mavazi asilia ya mwafrika? Ni nini muziki asilia wa mwafrika? Ni nini lugha asilia ya mwafrika? Ni nini dini asilia ya mwafrika? Zaidi ya maswali 67 bila majibu. Kama kawaida na desturi za kiafrika, hivi karibuni niliamua kutafuta majibu ya maswali haya kutoka kwa mababu na wazee waheshimiwa katika sehemu ya Afrika niliyozaliwa iitwayo Tanzania.

Ugumu ulianza kujitokeza mwanzoni tu mwa utafiti wangu. Wazee wengi walinishangaza kwa kunipa majibu ambayo hata wao wenyewe walikiri kwamba hawana uhakika nayo. Wazee wa Pwani wanadai kuwa lugha asili ya mwafrika ni kiswahili, dini asili ni uislamu, tamaduni ya asili ni ile yenye mvuto wa kiarabu, mavazi ya asili ni yale yanayofuata dini ya kiislam. Wazee wa kaskazini mwa Tanzania wanadai kuwa lugha asili ni kibantu, dini ya asili ni ukristo, tamaduni asili ni yenye mvuto wa kibantu, mavazi asili ni yale ya heshima kama waliyovaa wazungu wa kikoloni yaani suti na tai. Mchanganyiko wa ajabu. Kila mtu anasema kile anachodai kuwa aliambiwa na baba yake kuwa ndio asili ya mwafrika.

Haa! yaani asili ya mwafrika leo hii lazima iwe na mvuto wa kikristo au kiislamu! Yaani Tamaduni asili ya mwafrika ni ile yenye mchanganyiko wa kizungu au kiarabu! Ajabu! Ni nani leo hii atakayetuambia ukweli? Inaumiza zaidi pale mambo yanapokuwa magumu kama yaliyomkuta rafiki Yangu Dennis. Baada ya kuishi Marekani akisotea dola kwa miaka karibu minane, Dennis aliamua kwenda nyumbani januari mwaka huu.Cha kufurahisha zaidi, Dennis alikuwa amepanga kwenda kuoana na mchumba wake wa siku nyingi Natasha. Maskini Dennis akaenda kwa wakwe akiwa amesuka nywele zake na kuvaa heleni. Kwa mshangao wa wengi, wazazi wa Natasha walimzuia binti yao hata asikutane na Dennis kwa madai kuwa sio kijana wa heshima kwa vile amesuka na kuvaa heleni.

Cha kushangaza zaidi, wazazi wa Natasha ni wamasai! Yap,!! wamasai walokulia Dar es salaam. Hebu jiulize, heshima ya kijana wa kimasai ni ipi kimavazi? Dennis alinyimwa mke na akarudi Marekani kwa huzuni. Sitaki sana kuwalaumu wazazi wa Natasha kwa walichofanya. Tatizo lao ni kutojua kwa hakika asili ya mwafrika, mchanganyiko ulioletwa na waarabu na wazungu kwa waafrika ni wa kiwango kikubwa sana kiasi cha kumchanganya kila mwafrika leo asijue ukweli. Kila siku nasoma magazetini watu wakiwatukana madada zetu wanaovaa nguo fupi wakidai kuwa wanaiga utamaduni wa wazungu. Kila siku kuna watu wanawanyanyasa akina mama waliovaa mavazi yanayoonyesha maumbo yao huku wengine wakifikia hatua ya kuwapiga kwa visingizio kuwa mavazi hayo yanachochea dhambi! Dhambi? Nani ana uhakika? Ni nani baba wa kiafrika leo anayejua kwa hakika mavazi asilia kwa kila mwafrika kabla ya ukoloni? MWAFRIKA, NANI “DADDY” YAKO ?

Masikini mie, marehemu babu angekuwa hai ningemuuliza, marehemu baba angekuwa hai pia ningemuuliza. Bibi hana mengi ya kusema zaidi ya kuwa hakumbuki kuvaa nguo yoyote mpaka alipoolewa na babu. Na pia anakumbuka vyema kuwa babu alipokuwa kijana, alisuka nywele zake na kuvaa heleni kubwa sana. Bibi anakumbuka pia kuwa kivazi cha Kwanza alichovaa siku harusi yake iliyofanyika kwa mujibu wa mila za Kikurya, kilikuwa ni kipande cha ngozi kilichofunika sehemu za siri tu na sio zaidi. Huku akitabasamu, bibi anasisitiza kuwa miaka yake ya ujana, hakukuwa na vitendo vya ngono na magonjwa ya zinaa kama leo ingawa leo Wanawake wanavaa nguo zinazofunika kila sehemu ya miili yao. Umelipata hilo msomaji? Wanahistoria wengi wa kiafrika wanakubaliana kuwa waafrika wote walikuwa na dini zao kabla Wakoloni wa kiarabu kuja Afrika karne ya kumi na sita na kuleta uislam. Wanakubaliana pia kuwa , Wakoloni wa kizungu ndio walileta  ukristo Afrika mwanzoni mwa karne ya kumi na tisa.

Wanahistoria wengi wanakubaliana pia kuwa mavazi ya kanzu na kikofia yaliletwa Afrika na Wakoloni wa kiarabu, wanakubaliana pia kuwa mavazi ya suti na tai yaliletwa Afrika na Wakoloni wa kizungu. Ninaheshimu sana dini na imani za watu kwa hiyo sio kazi Yangu leo kuanza kuambia waafrika wenzangu kuachana na ukristo au uislamu. Lengo la makala hii ni kuwauliza wale wanaopayuka kila siku kwa kuchambua mavazi ya wengine kwa visingizio kuwa hayafuati mila na desturi za kiafrika wajibu kwa hakika kama wanajua mavazi asili ya mwafrika ni yapi.

Ni aibu na ni kinyume cha sheria kwa baadhi ya watu hasa wanaume kuanza kunyanyasa na hata kuwapiga Wanawake wanaovaa nguo fupi au zile zinazoonyesha maumbile yao. Ni utindio wa elimu kwa baadhi ya watu kuwasema vibaya na wengine hata kuvunja ndoa za vijana wa kiume wanaosuka au kuvaa heleni. Ni uzembe wa mawazo kwa baadhi ya wapiga domo Kulalamika kuwa mziki wa kizazi kipya wa bongo fleva asili yake ni Marekani bila ya kujali ukweli ambao unaonyesha kuwa wakurya wamekuwa wakirapu “Kuibhaka” kwa miaka zaidi ya mia na hamsini kabla wamarekani weusi hawajaanza kurekodi na kuuza rapu. Ni kupingana na historia kwa kwa baadhi ya watu kusingizia kuwa mavazi mafupi ya dada zetu yanazidisha vitendo vya zinaa wakati ukweli unaonyesha vinginevyo. Hebu tuache kupayuka na kusema ukweli, tusifuate tu mila na desturi ambazo tulipandikiziwa na Wakoloni bila kujiuliza umuhimu wake. Tuachane na mababu na wazee wenye majibu ya kubabaisha na tujibu swali hili kwa uzito wake, MWAFRIKA, “DADDY” YAKO NI NANI? Ni mzungu?, Ni mwarabu?, au ni Mwafrika Mwenzako ?

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.