TANGAZENI MIJI YA ZAMANI

Na, Antar Sangali, Bagamoyo

Mara nyingi kama sio zote Watanzania tumekuwa tukiimba nyimbo ambazo hukosa mantiki na wala haziendani kabisa na midundo ya ngoma tunazopiga iwe ni kisiasa. kijamii, au kiuchumi.

Walimwengu wamekuwa wakitucheka na kutushangaa ni kwanini tumekuwa waimbaji wazuri wa nyimbo zenye vina, pambio na mizani ya utungaji mahiri kuliko kufuata midundo halisi ya ngoma tunayoidhamiria kucheza na kutimbwirika. Wengi wanatushangaa, na pengine watazidi kutucheka! Wanatushangaa sana tena sana kwasababu aghalab tumekuwa watu wa maneno "miingi" lakini utekelezaji wetu hukumbwa na urasimu, umimi na sana hatujali maslahi ya Taifa kuliko mtu na kushiba kwa tumbo lake.

Nimekuwa nikifuatialia sana kauli mbiu za serikali yetu katika dhamira ya kuzitumia rasilimali zetu asilia na hasa katika nia ya kutangaza utalii na maeneo ya kitalii ikiwemo miji ya kitalii, mbuga za wanyama, makumbusho ya Taifa, mila, na utamaduni wa watanmzania. Lakini kadri miaka inavyozidi kutaradadi bado hatujaonyesha kama kweli tunakusudia na kuwa na dhamira ya wazi ya kuuinua utalii na kuzitangaza aidha mbuga zetu za wanyama, makumbusho na miji yetu ya kihistoria ambayo inahadhi mbele ya historia ya nchi yetu, Afrika Mashariki, Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

Nikitazama Mbuga ya Saadan ambayo ni ya kipekee (unique) miongoni mwa mbuga chache katika Dunia yetu, lakini hakuna jitihadi za kuitanzagza mbuga hiyo ambayo inatosha kuipatia nchi pesa nyingi za kigeni na kukuza uchumi.

Tazama mji wa kihistoria wa Bagamoyo ambao ni mashuhuri katika Tanganyika ya kale kwa biashara za watumwa , pembe za ndovu na manukato..., ukiunganishwa na njia ya watumwa "Caravan Route" toka sehemu za Tanzania Bara kule Kigoma -Ujiji , Tabora hadi Pwani yake. Bagamoyo ni lango Kuu lililokutanisha tamaduni, makabila, dini, na watu wa mataifa mbalimbali katika zama nyingi zilizopita.

Lakini leo ukiitazama Bagamoyo huwezi kukubali kama ukilinganisha thamani ya historia yake na uduni wa mji huo na watu wake walivyo maskini hohehahe! Bagamoyo ni chimbuko la Lugha ya Kiswahili na Dini za Kiislam na Kikristu toka Pwani na kuenea Bara ya ndani ya Tanganyika.

Aidha Bagamoyo ni "strong Base" ya chama cha siasa cha TANU katika kupigania harakati za uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 ikiwemo na Mikoa ya Kigoma, Tabora , Pwani na Dar es - Salaam.Lakini, tazama majengo mazuri ya kihistoria yanavyoporomoka, njia ya kupitishwa watumwa inavyozidi kuchaka, pia eneo ambalo mwili wa marehemu Dk David Livingstone alipolazwa ukitokea mpakani mwa Zambia na Afrika Kusini na kubebwa na wapagazi wake wa Chuma na Susi lisivyo-thaminika...!!

Bagamoyo ni mji wenye upana wa historia timilifu na yenye kumvuta mtalii yeyote atoke atokako na kufika katika mji huu ambao ni chimbukola ustaarabu unaofanana na Nchi ya Misri,ustawi wa dini za kikatoliki na kiislam ni mkubwa na una historia kubwa inayoweza kumtoa nyoka pangoni.

Bagamoyo ni mji ambao mapdri wa kikatoliki walijenga kambi maalum ya kunusuru watu weusi wasiuzwe katika soko la watumwa huko Zanzibar na wengine kukombolewa kwa kiasi cha fedha na kupewa uhuru kama watu na hazi zao za ubinadamu.

Mji huo sasa umepata mvuto mpya una msafara mrefu wa Hotel kubwa za  kitalii matahalan Paradise Resort,Travellers Logde,Oceanic Bay, Bagamoyo Beach, Palm Tree, The Malaika Livingstone Pink Shark, Sea Breeze Mellinium, Badeco Beach ni mji ambao unaonekana kukua upya kwa mwendo wa haraka kwa sekta ya utali na hasa bada ya serikali kuweza kuijenga Barabara yenye umbali wa kilomita 65 itokayo Dar es Salaam hadi Bagamoyo na hivyo kuifanya Bagamoyo kuwa karibu sana na Dar  kuliko miaka mingi iliyopita.

Ubalozi wa Sweden kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Misaada (SIDA) mwaka 2002 ulifanya kongamano la kimataifa lililokusudia kuuingiza mji huu katika orodha ya miji ya urithi wa dunia yaani "A World Haritage Sites" lakini cha ajabu juhudi hizo zimeonekana kuyayuka mithili ya barafu mbele ya jua la kiangazi..!!

Kakitazame kisiwa cha Mafia kina magofu ambayo yanasemekana yamejengwa kwa takriban miaka elfu iliyopita, ina mandhari njema inayovutia machoni sambamba na kuzunguukwa na Delta ya mto Rufiji huku pembezoni kukiwa na Mbuga kubwa ya Selous.

Saadan ni mbuga inayokutana na Bahari "A bush meet a Beach" mbuga ambayo inapacha za mito miwili ya Wami na Ruvu inayomwaga maji katika Bahari ya Hindi na ambayo samaki aina ya kasa hutaga kati ya nchi za Pwani ya Mashariki ya mbali na Pwani ya Bagamoyo, ni Saadan ambayo Bushiri Bin Salim chotara wa Ki-Oman na Kiafrika alipigana na Wajerumani akipinga kutawaliwa hadi alipokamatwa na kunyongwa hadharani mwaka 1889. Saadan ina baadhi ya wanyama ambao hawapatikani katika mbuga nyingine Tanzania na Duniani.Twiga wenye mabaka meupe na meusi na mbega wekundu wanaonekana Saadan tu.

Nimeitazama Kilwa mji ambao umebeba historia kwa uzito unaotimia. Mji ambao uliweza kuwa na sarafu yake katika miaka mingi dahari iliyopita. Ni mji ambao kuna Gereza moja la kihistoria "Gereza Fort" lilojengwa na Wareno katika mwaka 1505 na kukarabatiwa tena na Waarab mwaka 1807 , likiwemo pia jumba la Makutani "The Makutani Palace" , msikiti mdogo "The Small Mosque" sambamba na makaburi ya Washiraz ' Shiraz Tombs".

Kilwa ni mji ambao umehusika kuwa ni chanzo cha kuanza kwa mapambano ya vita ya Maji maji ilianza mwaka 1905 hadi 1907 na Kilwa kuna mapango makubwa ya kihistoria kwenye vilima vya wamatumbi ambayo ni mapango ya miaka 100 na ushee.

Inasikitisha sana kuona kuwa Taifa bado halijaona ubora na thamani ya miji hii ya mizuri ya kale!

Tazana kwa mfano wenzetu Afrika ya Kusini wenye miji mikubwa mathalan Johnesburg na Pretoria, kisha jiulize: ni kwanini shughuli zao za kitalii ikiwemo mashindano ya urembo wa dunia na zote za Afrika Kusini wazifanyie kwenye mji wa Sun City na siyo Durban au Johnesburg??

Jawabu ni rahisi:-Mji wa Sun City kutoka Johnesuburg ni umbali wakilomita 100 lakini kutokana na mipango endelevu wameuteua mji wa Sun City uwe kama kioo cha utalii na starehe na kama kitega uchumi chao.

Swali tunalopaswa kujiuliza ni hili: hivi ni kwanini tunaitazama sana Da es Salaam peke yake na kusahau miji mingine ambayo kama sisi wenyewe tunaipuuza nani wa kutujengea na kuitangaza?

Kila kitu kizuri Diamond Jubilee-Dar es Salaam,kila mwanamuziki mgeni ajapo nchini hupelekwa Diamond Jubilee. Hafla yeyote kubwa ya kimataifa na kitaifa Diamond Jubilee.Miss Tanzania huko huko! Kwanini!?

Hivi bado kweli tuna akili zile zile za kuijenga Dodoma kwa miaka lukuki huku Singida ikiachwa iko taaban!?

Kama kweli tunataka kukuza utalii basi hebu tuigeuze bongo,tutafute Bongo Mchicha tunayoitaka kwa maarifa na fikara mpya ili tuitangaze miji yetu ya kihistoria yenye kumbukumbu maridhawa kwa kupeleka hafla kubwakubwa mathalan Miss Tanzania zifanyike Bagamoyo,Mafia, Saadan au Kilwa.

Hii ni miji iliyoshiba historia rasilimali,hazina na amana zilizoko huko ni kumbukumbu za utalii tunaoutaka na kuimba kila kukicha huku kukiwa na juhudi za kusuasua.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.