TABAKA NA FIKRA ZA "SISI" NA "WAO"

Na, Edward chacha

Katika moja ya hotuba zake, Mwalimu Nyerere aliwahi kuonya kuwa:endapo kama tutaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za "Sisi" na "Wao" nakuwaacha watu wachache wawe na mali na nguvu, na fidhuli ya kuwa na mali na nguvu; na wengine wengi wawe ni maskini na wanyonge; wenye manung'uniko, na ghadhabu za umaskini na unyonge, itakuwa ni kosa kubwa sana ambalo litavuruga msingi wote wa utulivu na amani tunaojivunia leo hii.

Utaratibu wa Vyama Vingi katika mazingira na hali fulani unaweza usiathiri utulivu. Lakini tofauti kubwa sana za mapato au za hali ya maisha au hata za matumaini tu ya maisha mema ya baadaye, haziwezi kuzaa utulivu.

Wasiwasi kubwa inayojitokeza ni hatari inayoweza kutokea kwa umoja wetu endapo kama tutaendelea na hii tabia ya baadhi ya vigogo kujilimbikizia mali na kujijengea mahekalu ya kifahari huku wananchi wa kawaida hususani vijana wakisota kila siku bila hata ya kujua mlo wao wa kesho utatoka wapi.

Baya zaidi, wengi wa vijana hao hawana kazi na wako mitaani tu wakisubiri kichocheo cha fujo kitokee ili waweze kuyatoa hadharani mangung'uniko yao yaliyochanganyika na gadhabu za umasikini unaowakabili. Fujo za hivi karibuni huko Tanzania visiwani ni mfano mzuri wa kutizamwa.

Tusiipuuze hoja hiyo: umoja wa watu wetu ndiyo nguvu yetu kubwa kuliko zote. Hatari za mifarakano inayoweza kuzuka kwa misingi ya tabaka la "sisi" na "wao" lazima ziepukwe kwa namna yoyote ile. Na hili linawezekana kabisa kwasababu Tanzania sio nchi masikini kabisa kama baadhi ya viongozi wachache "manyang'au" wa chama na serikali walivyofanikiwa kuwafanya wananchi wengi wa kawaida wasadiki.

Iweje leo Tanzania yenye madini kiloba, mbuga za wanyama lukuki, ardhi bora nyenye rutuba ya kutosha, mito na maziwa makubwa barani Afrika ishindwe kabisa kulipatia suluhisho tatizo la ajira kwa vijana kwa takribani miaka 44 sasa tangu tuanze kujitawala? Huu ni uzembe mkubwa! Na kama sio uzembe mkubwa, basi wapo wajanja wachahe wanaokula hiyo keki ya taifa peke yao na kuwaacha mamillioni ya watanzania wakiishi maisha magumu ambayo yangeweza kuepukika endapo kama hao "wachache" wangeweka kando "unyang'au" wao na kuweka mbele maslahi ya Taifa.

Lau tukiondoa ubinafsi, na kisha rasilimali hizi zikatumiwa vizuri Katika jitihada za kuinua hali ya uchumi ya wananchi wa tabaka la chini kwa kuongeza ufanisi na ari ya kufanya kazi kwa kubuni miradi na shughuli zitakazotoa ajira kwa wale wasio na ajira; watu watajipatia mapato ya kujikimu na hatimaye hali na hadhi zao za kimaisha katika jamii zitaongezeka. Hali hiyo ikitokea (vijana wengi wakapata ajira ya kudumu), hata kama vigogo sasa wakiamua kujilipa mishahara minono, na kujiongeza marupurupu, then poa tu. Manung'uniko unayoyasikia sasa hutayasikia tena.

Upende, usipende, hatari iliyoanza kujitokeza waziwazi kwa sasa ni mgawanyiko wa "Sisi" na "Wao" katika tabaka za kiuchumi na kijamii. Kwa wale vigogo walioko serikalini wanazidi kujineemesha kupitia migongo ya masikini walalahoi kwa kuiba na kujilimbikizia mali nyingi iwe ni kwa style ya 10% ama wizi wa kimachomacho. Wakati huohuo wananchi walalahoi wa kawaida wakizidi kupiga hatua kurudi nyuma bila hata ya huduma za msingi za kijamii.

Kama Mwalimu alivyowahi kuonya: "Tofauti kati ya watu maskini na watu matajiri zinaongezeka Tanzania. Inafaa tuwe macho. Ni lazima tuendelee kutumia Sheria za nchi, na mipango mbali mbali ya Serikali, kuona kuwa tofauti hizi hazifikii kiasi cha kuhatarisha umoja na amani katika nchi yetu. Na hasa hasa ni lazima tuendelee kuhakikisha kwamba mahitaji ya msingi ya watu wote yanapatikana na yanalindwa. Lengo letu lazima liendelee kuwa kuinua hali ya maisha ya kila mtu, na kila mtu aweze kupata huduma za msingi za elimu na matibabu. Maana kama watu wachache wanaishi maisha ya fahari fahari, na watu walio wengi hawapati hata mahitaji yao ya lazima, hatutaweza kudumisha amani na utulivu nchini mwetu. Ni muhimu sana kwa Chama tawala na Serikali zake kulizingatia jambo hili kwa makini."

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.