UMOJA NA MSHIKAMANO WETU.

Na: Antar Sangali, Bagamoyo <modified on: 03/11/10>

Taka tusitake, Falsafa "unganishi" za Mwl Nyerere zitazidi kuiongoza Tanzania na Afrika kwa muda mrefu sana wakati yeye akiwa Kuzimu...; Tathmini na uchambuzi wa kutosha kisiasa umeonyesha na unazidi kuonyesha kwamba hayati Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Tanzania alikuwa ni mwanasiasa mwenye upeo mpana, akili zilizotimia na aliye na maarifa ya kotosha katika kubaini mambo yajayo kulingana na hali ya wakati ulivyo na bila shaka wadadisi na weledi wa masuala ya siasa wanadai alizaliwa na kufa kama kiongozi wa watu na kimsingi Nyerere ni mwanasiasa wa karne.

Ni miaka mitano leo imepita tokea uhai wa Mwalimu Nyerere ulipokatika kutokana na mardhi ya saratani ya damu na kufariki katika hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza mwaka 1999, lakini bado falsafa zake zinazidi kuiongoza Tanzania pamoja na sehemu kubwa ya Afrika.

Nimekuwa nikijiuliza na kushindwa kupata majawabu ya haraka haraka ni kwanini sauti ya Mwalimu imekuwa ikisikika katika vipindi mbalimbali vya Televisheni, Radio na kusomeka makala zake mbalimbali katika magazeti na vitabu vya waandishi mahiri duniani na husuasa hapa nyumbani Tanzania.

Binafsi nilikuwa nampenda sana Mwalimu Nyerere tokea nikiwa na umri mdogo na hata nilipokuwa nikisoma shule ya msingi na sekondari mara kadhaa nimejifunza mambo mengi kupitia maisha, misimamo na hutuba za Kiongozi huyu shujaa.

Kilipotokea kifo chake nilikuwa kama mtu niliyepatwa na mzubao wa akili na hasa wakati ule nchi hii Tanzaania ikiwa na uchanga wa mfumo wa siasa za vyama vingi na Mwalimu alikuwa ni tegemezi Kuu la watanzania werevu katika upambanuzi kutokana na ugwiji aliojaaliwa wa fikara na upeo wake katika masuala muhimu hasa ya kisiasa.

Laiti nisingelikuwa na dini yangu ambayo imenifunza kujua kuwa kila kilichoumbwa na Mungu kitakufa na iko siku ya hukumu mbele ya mungu nadiriki kusema leo hii ningelikuwa tayari ni mwenye kuteleza kwa kuamini kwamba ni basi asingepatika mtu anayeweza lau kufikia theluthi ya akili alizojaaliwa Nyerere na Mungu wake katika kuliongoza Taifa.

Nimekuwepo nchini Ethiopia kwa miezi kama minane na ushee mwaka 1991 katika mji mkuu wake Adis Ababa baada ya kupita katika miji ya Isiolo na Marsabiti nikitokea Nairobi Kenya na hatimaye kuingia mpakani Moyale, Kenya na na kuweza kupita katika miji ya Mega, Dila, Shashamanne hadi Adisababa, Ethiopia. Nikiwa katika kijiji cha Shaashamanne nimetumia muda mwingi kuzungumza na rafiki yangu aitwaye Fetuni Tadese nikimdadisi hali ya kisiasa na maendeleo ya mji wa Adis Ababa kiuchumi na kijamii.

Fetuni kijana wa Kiethiopia toka kabila la Amharic aliyepata elimu katika Chuo Kikuu cha Ethiopia aligeuza macho yake mara kadhaa akinitazama kwa macho makali yaliofanya kama ishara ya kunikataza nisiwe mwenye kudadisi maneno ya siasa lakini akili zangu zilinituma kufanya hivyo bila ya hofu.

Nilipomuona si mwenye kutamani mazungumzo hayo tuyape nafasi, zilinijia akili kwamba naweza kuzungumza naye nikiwa katika kupata kilevi katika Baa yeyote tulivu katika mji huo wenye Marasatafari wengi na kuishi katika maisha yale ya Kiafrika asilia. Kiu yangu ni kutaka kuujua Adis ikoje na nitaiingia vipi na kuishi ili kufikia azma yangu ya kwenda nchini Sudan au Djibout na kisha nifike Misri kwa kuelekea Ugiriki baada ya waya mkali wa maisha katika Bongo ile kavu ya Kujenga Ujamaa na Kujitegemea.

Fetuni alipokata chupa tatu za bia, akalazimika mwenyewe kuiamsha mada yetu na kuniuliza kama niliwahi kufanyakazi za upelelezi na usalama wa Taifa na vipi nilitumika katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Swali lilikuwa gumu kwangu na hasa nikiwa na miaka michache toka nimalize elimu yangu ya sekondari lakini nikasema ikiwa nitashindwa kujibu lolote basi nitakuwa ni mwenye kufeli mtihani nilioukusudia kuufanya kwa ridhaa yangu mwenyewe.

Nilimjibu swali lake ingawaje nami nilijibu katika hali ha hanjamu na sanifu za kilevi lakini naamini nilimjibu kwa utulivu na umakini uliomshawishi aingie katika uwanja niliokusudia awemo.

"Ukombozi wa Afrika na Uhuru wa Tanzania mwaka 1961 hakuna anayeweza kijigambana kuonyesha kidole chake juu kama ameuleta yeye na nguvu zake, bali ni juhudi za pamoja, mimi nilipigana nikiwa shuleni hivyo ni wazi nikisema nilipigania uhuru na ukombozi" nilijibu kama Mjivuni.

Tadese aliniuliza tena "Nchi yenu ina makabila na dini ngapi Kuu na vipi Julius Nyerere kama anapendwa na kufuatwa kwa siasa zake za Ujama kama ilivyo Ethiopia chini ya Mengestu Haile Mariam?" aliuliza.

Nilimjibu bila kuchelewa kwamba anapendwa sana kwasababu ameleta uhuru bila ya umwagaji wa damu, kuna dini mbili kuu lakini kuna watu hawana dini na hawataki dini lakini wana haki sawa mbele ya jamii, katiba na sheria za Tanzania. Ujamaa Tanzania sio Issue tatizo ni ajira na maisha duni, uchakavu wa barabara na uchache wa shule za Msingi na sekondari na kilimo duni kinacholeta njaa katika ardhi kubwa yenye rutuba na mito kibao ya kumwagilia.

"Mnaishi vipi na kugawana madaraka ya utawala serikali chini ya lundo hilo la makabila na uko wapi hapo uwakilishi sawia wa dini zote hizo huoni kuna watu wanaonyimwa haki na fursa ya kushirikishwa" aliuliza Tadese na kusema si kweli kama Rais Nyerere anapendwa kama nilivyomwambia awali.

Nilipojaribu kumsaili kwamba ni vipi makabila yanaweza kuwa kikwazo katika uendeshaji wa nchi na kuwagawa watu katika Taifa moja alinambia nchini kwao ni mtihani mkubwa kwani kuna makabila mawili makubwa ya Amharic na Tegry na hivyo ni upendeleo na kubebena tu.

Katika hali ya kunistaajabisha alitamka bayana kuwa kabila la Amharic ni la watu werevu, wenye upeo, waungwana na ambao wanafaa sana katika kushika utawala kuliko kabila la Tegrey na kwamba wategrey ni watu wasio na ustaarabu na hata nitakapo kuwa Adis niwatahadhari sana. Ghafla Tadese alikatisha mazungumzao yetu na kunibonyeza kwamba mtu aliyekaa nyuma ya kiti changu ni askari kanzu na kanambia haraka haraka "Zip your mouth" na mimi nikanywea kama uyoga.

Nilipofika Sudan katika mji Mkuu Khartoum mwaka 1991 mwishoni, nikajifanya mchokozi na kutaka kujua vipi mizungu ya siasa katika nchi hiyo inavyochezwa na maisha ya watu wake kwa ujumla wanavyoikabili katika michakato yao ya maendeleo.

Rafiki yangu aitywaye Mubarak Turabi raia wa Sudan ambaye nilipata kukaa naye selo katika kituo Kikuu cha Kati cha Polisi Adis Ababa kwa kosa la kuingia bila ya visa akanikataza katakata nisizungumzie siasa katika nchi hiyo na kusema "acha siasa, abudu Mola wako, siasa si hasa, khali abuu yaani achilia mbali" alisema Mubarak. Lakini jioni akanitaka tuende akanionyeshe watu wenzangu mahali wanakoishi na kusema si vibaya vile vile tukipata kinywaji mahali fulani.

Nikamuuliza tupate kinywaji hali nawe uko katika vazi la kidini, huoni aibu ! akacheka sana na kusema kipindi cha kusali sheikh kikimalizika chochote kinawezekana usiku!! Mubarak alizidi kuniambia kuwa siasa si kitu adhim na ambacho kimeweza sana kuyaharabu maisha ya watu na vilevile kuwatenganisha marafiki wakubwa walioshibana na kuthaminiana kwa miaka mingi dahari bora ya kuthamnini na kuifuata dini na hasa dini ya kiislam na kwamba dini nyingine zote si dini halali.

Nilipokuwa nchini Uganda mwaka 1992 mwanzoni niliwahi kuishi kwa wiki moja nyumbani kwa Bwana mmoja katika mtaa Mengo Hill aitwaye Haji Abdulmale raia wa kiganda mwenye asili ya Kihindi.Naitambua Kampala, Jinja ,Tororo na Mbale nimekutana na makabila ya huko wakiwemo wa-Acholi na wa-Baganda na kuutazama uislam na ukristo ulivyo katika nchi hiyo ambayo ilipata uhuru wake mwaka 1962 chini ya marehemu Dk Milton Apolo Obote.

Waacholi na Wabaganda ni makabila makubwa lakini kila kabila linaliponda kabila jingine kwa madai yale yale ya ubwana na utwana, ustaarabu na jingine ni la kishenzi kwa mitazamo yao hafifu isiyo na mantiki.

Kadhalika nikiwa Uganda nimeshuhudia baadhi ya wananchi wake wakimshutumu Obote kwa kuwakandmiza sana waislam katika utawala wake na kumsifia Idd Amin Dada jinsi alivyokuwa anaupenda uislam na kwamba shutuma nyingi za ufashisti dhidi yake ni za kupika lakini hazina ukweli kama alizofanya Amin au maswahiba zake serikali zikiwemo za mauaji ya kimabari.

Nimekuwa pia Nairobi Kenya mwaka kati ya miaka 1988 na 1991 na kuishi na wakikuyi na wajaluo, sana sana nimekaa na wameru na wakamba kwasababu ni wauza miraa wazuri na mimi hupenda sana kula Gati hasa niwapo Kenya huku TZ ikipiga marufu miraa na Kenya wenzetu ikiuza na kupata mamilioni ya Ngawira za Kigeni.

Nimewashuhudia wakipuuzana na kukebehiana jambo lililonifanya mara chungu nzima kumkumbuka Nyerere na siasa zake zilozolenga umoja wa kitaifa na kupiga vita ubaguzi na udini.

Wakenya na siasa zake hutegemea sana nguvu ya ukabila na wanasiasa wenye mitaji ni wale wanaotoka kwenye makabila yenye watu wengi mathalan Wakikiyu na Wajaluo "Abaluya na Luo Union"

"Ni heri uwe na dini lakini usiaathiriwe na virusi vya udini, na ni afadhali mara elfu uwe na kabila lako ili kujua namna ya kufanya matambiko yenu na kujua watani wako ni makabila gani kuliko kuwa na hisia na kuwa mkabila" alisema Mwalimu Julius Nyerere katika maisha yake.

Mwaka 1999 nilikuwa nakwenda kuhudhuria kongamano la kimataifa la 49 la Liberal International mjini Brussels nchini Ubeligiji. Nimekutana na kijana mwenzangu uwanja wa ndege Dar es Salaam na kisha tukawa wote Jomo Kenyatta Air Port Nairobi, Kenya hatukuulizana makabila zaidi ya vipi mzee unatoka Bongo jibu likawa ndiyo mzee.

Nimekutana na Stephen Mnadalila kijana aliyekuwa akienda nchini Marekani masomoni zaidi tuliulizana "mshikaji unaishi wapi" akasema kwao Temeke Dar na mimi nikwamwambia kwetu Kibaha Pwani. Lakini huwezi kuamini mshikamano wetu ulikuwa katika kamba ile ile ya huyu ni "ndugu yangu" "Mbongo mwenzangu" cha ajabu mpaka leo tunaishi na kuwasiliana kama ndugu tuliofahamiana miaka mingi sana iliyopita.

Nikiwa mdogo na hata nilipomaliza kusoma shule ya sekondari niliingiwa sana na itikadi ya kumpenda mwalimu Nyerere alinivutia sana wakati akija na wageni mbalimbali wa kimataifa katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Ruvu kikosi cha 832 kwenye miaka ya mwishoni mwa 1969 hadi 1978 wakati huo Mkuu wa Kikosi akiwa Jenerali Mkame Rashid Nnalihinga sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Niliwahi kumuona mwalimu akija Ruvu akiwa na Rais Siaka Stephen wa Siera Leone, Mfalme Mshoeshoe wa III wa Lesotho, Olusegune Obasanjo wa Nigeria, Fiedel Casro wa Cuba, Samora Machel wa Msumbuji, France Albert Rene wa Sychells na marais kadhaa nilowasahau. Naeleza haya nikionyesha kwako msomaji wa mkona hii ya Bongo Mchicha ni vipi mwalimu alihusika kunivuta katika itikadi ya ke kisiasa ,hotuba zake, misimamo yake iwe ile ya kitaifa na kimataifa na ushawishi aliokuwa nao katika kufikisha ujumbe kwa watu wake na walengwa aliowakusudia kwa wakati autakao yeye mwalimu.

Mahubiri ya Mwalimu mara zote kwenye majukwaa ya kisiasa na katika medani za kimataifa yalikuwa ni kama wimbo wataifa kuhusu hatari na athari za ukabila, udini na ubaguzi wa rangi. Alionyesha jinsi alivyokuwa akichukia kwa nguvu zake zote na kuvipuuza vitu hivyo sikuzote za uhai wake.

Mara chache kama si zote nimekuwa nikijiuliza hivi huyu Mwalimu Nyerere hukuwa na jingine la kuwaambia watanzania zaidi ya ukabila, udini na ubaguzi wa rangi na la ziada ukiongeza katika mahubiri yake ni ujenzi wa siasa safi ya ujamaa na kujitegemea na kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa--basi! Hana jipya ? Lakini wahenga wa kiswahili walinena tembea ujionee, na tembea ujifunze kwani nilipokuwa katika matembezi yangu ndipo nilipoona kuwa Mwalimu alikuwa akiona mbali ambako hata marais wenziwe katika Afrika mara baada ya uhuru wa nchi zao laiti wangehimiza mambo hayo ni dhahiri leo vita, ukabila na hisia za udini zingekufa na kufutika kwa kiasi kikubwa Barani Afrika.

Jafari Nimeir hakufanya hivyo Sudan, Mangestu Haile Mariam aliukwepa wimbo huo wa Nyerere kule Ethiopia, Siade Barre kadhalika aliupa kisogo wimbo huo Somalia, na Dk Milton Obote hakuucheza kabisa wimbo huo akiwa Uganda. Tumeshuhudia kwa macho yetu yaliyozipata nchi za Burundi, DRC na Rwanda kwa kususa kuimba wimbo huu.

Hotuba za Nyerere zinatawala katika TV za Bongo, Siasa za Bongo, maisha ya kijamii katika Bongo na zitaiiongoza Tanzaia na Afrika nzima ilhali yeye mwenyewe akiwa ahera -Kuzimu- kwakuwa ni hotuba zenye uhai, ujumbe, thamani, mantiki na taaswira endelevu. Viongozi wa Tanzania mliopo na mjao mtizameni na muigeni sana Mwalimu, amefariki lakini uzito wake bado unaibeba nchi yake na Bara zima la Afrika na ameliandika jina lake kwa wino wa dhahabu usiofutika milele katika mlima mrefu uitwao Kilimanjaro kila asiye na macho atazame ataona. Ukiona kilima Kilimanjaro utaiona Tanzania, ukilikuta Taifa hili utaiona misingi ya amani, demokrasia na utulivu usio na chembechembe za ukabila, udini zaidi utaliona Taifa lililo na umoja wa kweli wa Kitaifa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.