*UJASIRI WA SUMAYE NI PESA*

Na, Padri Privatus Karugendo <14/08/05>

Sasa hivi ni wakati wa kuwapamba marais wetu watarajiwa. Ni wakati kumpamba Sumaye. Yeye ni mnyenyekevu. Walio karibu naye wanaungama wazi kwamba mheshimiwa ana unyenyekevu wa hali ya juu. Hii ni sifa muhimu sana kwa nchi inayotaka kutunza amani na utulivu bila kuzingatia mambo mengine kama uchumi na utawala bora. Watu waendelee kuongelea kwenye umasikini huku wakiimba wimbo unaochefua wa amani na utulivu ni nguzo za taifa letu.

Sumaye, ni mvumilivu. Amejaliwa kipaji na mwenyezi Mungu, kuwa mvumilivu. Amevumilia maadui zake, hata na wale waliokuwa wakimpaka matope.Yeye mwenyewe anasema:

"Wapo wanaoamua kuwachafua wengine ili kutimiza malengo yao ya kisiasa, huu si ustaarabu. Unapotumia mbinu hiyo, maana yake mwenzako anakuzidi nguvu, kwani kama hakuzidi, ni kwa nini umchafulie?...Mimi siwezi kumhujumu mtu na wala sitamchafua mtu".

Hawezi kulipiza kisasi. Amekuwa kwene nafasi ya juu serikalini. Alikuwa kiranja wa mawaziri, hatujasikia akijilipiza kisasi. Katika nchi kama Tanzania , inayotanguliza amani na utulivu na mshikamano, huyu ndiye anayefaa. Atashughulika na amani na mshimamono na kuwaachia wawekezaji wasombe kila kitu.Apite Sumaye! CCM, juu!

Sumaye, ana uzoefu wa muda mrefu katika siasa. Taifa kama Tanzania, linalotanguliza amani, utulivu na mshikamano, linahitaji rais mwenye uzoefu wa muda mrefu katika siasa. Elimu si jambo muhimu, hata Iddi Amin, aliitawala Uganda na kuiacha historia nyuma yake, yeye Sumaye anasisitiza jambo hili katika mahojiano aliyofanya na gazeti mojawapo siku za hivi karibuni:

"Sidhani kama suala la elimu ndicho kigezo kilichopo. Ni watu wanaonisema. Hata katika chama chetu tunasema mgombea awe na elimu ya chuo kikuu au inayolingana nayo. Sasa kama ni suala la elimu, mimi ninayo inayolingana na hiyo, kinachotakiwa zaidi ni uzoefu wa uongozi. Nimekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, nadhani hayo ndiyo muhimu".

Kama tungekuwa na mfumo mzuri wa demokrasia, tungemuuliza Mheshimiwa Sumaye, miaka yote katika siasa imezaa nini. Haitoshi kukaa miaka mingi katika siasa. Jambo la muhimu ni umefanya nini katika siasa. Kuna watu wanakaa muda mfupi katika siasa, lakini kwa vile walikuwa na vision na kusimamamia maoni yao katika jamii, wanakumbukwa kwa miaka mingi, wanaandika historia isiyofutika. Kennedy, hakuitawala Amerika kwa miaka mingi, lakini hadi leo hii anakumbukwa. Kwa vile sisi tunaongozwa na pesa, basi Sumaye, anaweza kusema lolote, na kupata kura! Si kwa sifa zake, bali kwa pesa zake! Cheka kama unataka na lia ukijisikia kulia, ukweli ndo huo!

Sumaye ni mtiifu. Tumeabiwa amemtii kwa kiwango kikubwa rais Mkapa. Huyu ndiye rais tunayemtaka. Alivyo mtiifu, ndivyo atakavyotaka wengine wamtii. Vioongozi wakimtii, wakifuata kila anachokisema " Ndiyo mzee", nchi itakuwa na amani na utulivu.

Sumaye, ni rafiki wa karibu wa rais Mkapa. Huyu atamtunza vizuri rais wetu mstaafu. Hatupendi mpendwa wetu apate yale yaliyompata Kaunda na Chiluba.Tungependa mzee wetu akapumzike vizuri kule Lushoto, kwenye hewa safi bila kusumbuliwa na malalamiko ya walalahoi.

Sumaye, ni mcha Mungu.Tunakutana naye kanisani. Amekuwa mwaminifu kuhudhuria sherehe zote za kidini. Ziwe za wakristu au waislamu. Imani yake ni imara. Hatujamsikia kuhama kanisa lake la KKKT na kujiunga na makanisa mengine. Hatujamsikia akihama dini yake ya ukristu na kuingia uislamu au kutembelea Bagamoyo!

Sumaye ni kijana, ukimlinganisha na "Babu". Kuna msemo ya kihaya: "Abafu, bakilana okunuka", Tafsiri ya harakaraka: Maiti huzidiana kwa harufu mbaya.

Ingawa kampeni za Sumaye na "Babu" ni za kutumia nguvu ya pesa, pesa za "Babu" zinanuka zaidi, kuna mashaka kama zinaweza kuleta amani na utulivu.

Sumaye ana sifa nyingi! Labda Jesse na wenzake wanafikiri ninaandika haya nikilia na machozi yakidondoka. Si kweli! Ninaandika nikicheka. Ninafanana na mtu anayejinyonga kwa kamba aliyoitengeneza yeye mwenyewe. Ni lazima mtu huyu afe akicheka. Hata shujaa Mkwawa, alikufa akicheka. Kicheko cha huzuni na kujilaumu, dalili za kuonyesha ushujaa wa kijinga na ubwege! Maisha ni kitu muhimu, ukishayapoteza ni mwisho. Hekima ni kuyalinda maisha na wala si kuyapoteza!

Huu si wakati wa kulia. Hata tukilia haitasaidia kitu. Ni wakati wa kucheka kicheko cha huzuni na kujilaumu. Ni wakati wa kujinyonga kwa kamba tuliyoitengeneza sisi wenyewe.

Huu ni wakati wa kufikiria jinsi ya kubadilisha mfumo wa siasa katika Taifa letu. Ni wakati wa kukaa chini na kuandika katiba mpya ya taifa letu, ili tuachane na katiba iliyojaa viraka. Ni wakati wa kubuni mbinu za kuendesha uchaguzi wa haki. Uchaguzi utakaowaingiza watu madarakani kwa kufuata sifa na uwezo wao na wala si kwa kutumia pesa.

Nina imani akina Jesse Kwayu, wameupata ujumbe wangu. Ujasiri wa Sumaye, ni pesa. Kama kuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kumpokonya Sumaye, ujasiri wa pesa, kuipokonya CCM, ujasiri wa pesa na kuwapokonya wawekezaji ujasiri wa pesa, na kama kuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kuipokonya CCM, uwezo wa kutumia vyombo vya dola wakati wa uchaguzi mkuu, tunaweza kujadiliana juu ya ni nani ataingia kwenye viatu vya rais Mkapa. Kinyume na hapo hakuna mjadala. Mwenye nguvu mpishe! Mnyonge ni mnyonge daima hadi pale anapofumbua macho na kusema hapana!

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.