MUSTAKABALI WA TIFA LETU

Na, Antar Sangali (Bagamoyo)

Hebu na tuitazame ile nchi ya Tanzania,iliyokuwa Tanganyika chini ukoloni wa kiingereza,nchi ambayo machifu na watemi wake wa makabila mbalimbali walikataa katakata kutawaliwa na Wajerumani na hatimaye kupigana vita, Bushiri Bin Salim aliongoza vita hiyo kule Saadan Bagamoyo, Kinjikitile Ngwale akashika usukani Kusini mwa Tanzania Kilwa ,Mkwawa shujaa nyanda za juu huko Iringa na Mangi Meli wa Kilimanjaro kaskazini mwaTanzania .

Ukweli ni kwamba:Tanzania ni taifa linalotajika kwa kujaaliwa rasilimali chekwa za kimaendeleo ambazo wachumi wenye fani wanaamini kinadharia ya kuwa Tanzania ina silaha kali za kuufukuza na kutokomeza kabisa umasikini uliowaganda watu wake miaka 43 sasa tangu uhuru wa December 9,1961.

Tanzania iliyotajika kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi toka asilimia 3.6 mwaka 1995 hadi kufikia asilimia 6.7 mwaka 2005 na ambayo mfumuko wa bei umepungua toka takriban asilimia 22 mwaka 1992 hadi karibu asilimia 4.4 hivi sasa.Pato la mtu mmoja limeongezeka kutoka karibu USD 120 mwaka 1980 hadi 280 kufikia mwaka 2004. Kwa upande mwingine pato la Taifa yaani (GDP) limekuwa likiongezeka wastani wa 5.6 asilimia katika kipindi cha mwaka 2000-2004. Mapato yameongezeka kutoka USD Milioni 172.22 mwaka 1977 hadi kufikia USD Milioni 250 mwaka uliopita. Hizi ni juhudi na jitihadi za makusudi zilizofanyika katika kuratili Dira ya Maendeleo ya nchi. Dira ya mwaka 2025 ambayo ni matokeo ya juhudi za kitaifa inaonyesha upeo wa ustawi lakini ikikabiliwa na utekelezaji hafifu na pengine wenye kukwamishwa na baadhi ya viongozi wachache waroho wasiotaka keki ya Taifa igawanywe sawa kwa raia wote wa Tanzania.

Lakini kwa upande mmoja hakuna uwekezaji wa kujitosheleza na wenye tija katika kusaidia utekelezaji wake huku upande mwingine wa sarafu, sera ya pamoja na program za shirika la Fedha Duniani/Benki ya Dunia(IMF/WB) zimeonekana kupingana kinagaubaga na dira ya 2025.

Kimsingi picha inayopatikana na hasa ukitazama ustawi wa amani na utulivu wa Tanzania kwa miaka 43 ya uhuru toka mwaka 1961 ni dhahiri utabaini rasilimali za nchi hazitumiwi/hazitumiki na kama zinatumiwa na kutumika zinawanufaisha wachache na pengine niite ni "vigogo serikalini" na si kutazama maslahi ya masikini hohehahe watanazania wanaoishi vijijini ambako kuna huduma duni za ustawi wa jamii, afya, maji, barabara, zahanati na matibabu.

Rasilimali zilizomo Tanzania zilizoanza kutumika/kutumiwa na ambazo hazijaguswa na kuanza kutumika zinaweza kuifanya Tanzania yaani hii nchi ya Bongo kuwa Bongo Mchicha yenye ustawi bora maisha, masikini wachache, watu walioerevuka kwa kupatiwa elimu bora, yenye wataalam waliobobea katika fani tofauti, idadi kubwa ya viwanda, huduma bora za afya , hospitali zenye madaktari mabingwa na vifaa vya kisasa.

Kinachosikitisha ni kwamba:Watu toka mataifa mbalimbali wasomi wa fani na wanasiasa mahiri wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kama:-ni vipi Tanzania imekuwa ombaomba na kubakia mkiani mbele ya mataifa mengine ambayo yanakabiliwa na vita ya miaka kwa miaka, uchache wa rasilimali, na nchi nyingi kutokuwa na ardhi zenye rutuba kuliko ardhi ya Tanzania. Majibu ya maswali haya aghalab hubaki katika parandesi na hayajibiki kwa wepesi na kwa ufasaha unaostahili mbele ya nyuso za watu wastaarabu,waliosoma na kufuta ujinga na pia kwa wale wahisani na wafadhili wanoisadia nchi hii ya Tanzania kila kukicha kwa kigegezo cha " utulivu na amani" ya kudumu.

Mwaka 2005 ni mwaka wa uchaguzi Tanzania yenye jumla ya vyama vyoe 17 vya siasa vimeingia katika mbio za kuwania medani za kisiasa kwa kutaka udiwani,ubunge na Urais wa kuongoza dola kuelekea 2010. Watanzania walioamka wanaitamani nchi yao,urithi walioupata toka kwa akina kinjikitile na Mangi Meli na wengine waliomwaga damu yao kwa kuililia nchi hii ijitawale na itumie rasilimali zake kwa maendeleo yao na vizazi vyao.Watemi na Mchifu wetu waliwakataza kwa kupigana vita wakoloni wasiibe pembe za ndovu, ngozi za chui, mamba, dhahabu,almasi katika ardhi yetu ili zilifae Taifa hili na vizazi vijavyo. Matunda haya kamwe si miliki na urithi wa Chama fulani cha siasa na utawala wa aina moja ,ni miliki na hazina ya Taifa na watu wake bila ya kujali aina ipi ya chama cha siasa kimo madarakani na kutawala.

Lakini hili halionekani katika Tanzania ya sasa bali linalodhihiri ni kundi la watawala wachache wakipania kuidhinisha matakwa yao kwa kuzitumnia rasilimali zetu kwa kujinufaisha wao na familia zao.

Mpaka hivi sasa,vyama tisa vimesimamisha wagombea kutaka nafasi ya urais. Chadema, DP,CUF, CCM, NLD,TPP-Maendelo, NCCR-Mageuzi,TLP na SAU vyote makelele yao ni kutakakutumia rasilimali kwa faida za umma na kujenga ustawi wa maisha bora ya watu. Lakini ukivitupia macho vyama hivi unaweza kukata tamaa na pengine unaweza useme hakuna haja abadan ya kufanyika uchaguzi na kama unafanyika ni kutaka kujifurahisha na demokrasia katika kutimiza domokrasia-Makengeza na demo-ghasia mjini na vijijini.

CCM kama Chama Tawala ndicho kinacholalamikiwa kwa uharibifu na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, kuidhinisha na kuridhia mikataba ya ghiliba kuliko ile ya Karl Peters wa Ujerumani na machifu wa Makabila ya kiafrika amabyo haina faida wala tija yeyote kwa watanzania kwani wanachokibeba wawekezaji katika ardhi yetu ni kingi kuliko maslahi wanayopata wananchi ambayo hayana kipindi kirefu cha maendeleo katika maisha yao na kizazi kijacho.

Ukigeuza macho na kuutazama upinzani unaweza kutema mate na kuona kichefuchefu na ugegezi ukitanda kinywani kwani huko ndiko makundi ya walafi wa ruzuku walikopiga kambi,kufukuzana kusikokwisha na ukiukaji wa katiba zao na dhihaka kubwa ya demokrasia katika vyama hivyo.

Katika kambi ya upinzani Mwenyekiti na Katibu ndiyo wenye sauti na mamuzi na hawataki kupingwa lau kwa nguvu ya hoja ili kujenga mustakabali wa chama kisichofanana na CCM na kuwatia moyo na ari watanzania kuamini vyama hivyo vinahitaji mabadiliko aidha ya kiuchumi, kisiasa na kidemokrasia.Ni ving'ang'anizi wakuu wa madaraka ndani ya vyama hivyo vya siasa hawataki abadani mabadilko ya uongozi wakiaamini kuwa wao ni waanzilishi na kutoka kwao ni kuruhusu kundi jipya la uongozi kujipatia ruzuku ya ubwete ambayo hawakuisumbukia.

Kudumu kwa CCM katika madaraka kwa miaka mingi pengine ni matokeo ya kujisahau kwao katika kuutumikia umma kwa njia za usahihi na uwajibikaji chanya,lakini unaweza kupata kitete unapoutazama upinzania na mustakabali wake ni wazi unaweza useme kheri ya Mussa kuliko ya Firauni. Domokrasia au Domokrasia katika Afrika na njaa za viongozi wetu zisizo na sumile, uroho wa madaraka na ulafi wa kuiba usio na ashakumu kwa mali za serikali ni hofu juu ua hofu na sijui kama inaweza kupatikana Bongo Mchicha tunayoitaka na tunayoiona inawezekana na kuwa yenye neema stahili mbele ya watanzania wa mjini hadi vijijini.

Tanzania inahitaji kuwepo kwa utawala bora wa sheria huku watawala na watawaliwa wakijua maana ya kuheshimu na kutii haki za Bianadanu, uwajibikaji, ushirikishwaji, uwazi na ukweli na uhuru wa watu kusema na kukosoa kwa sauti ya juu ya kujenga bila ya kuchochea na kuhatarisha mchakato mzima wa ustawi wa amani. Hatutoweza kamwe kutumia rasilimali zetu kwa mizania iliyo sawa ikiwa mikataba ya wawekezaji ina kuwa na usiri mkubwa huku dhamana na maslahi ya Taifa anayekabidhiwa hatakiwi kuhojiwa na kuulizwa ni vipi ameafiki na kuridhia.

Watanzania wana haki ya kuamka na kutanabahi ni vipi ndani ya chama tawala wanaweza kubaini ujinga na uzembe uliomo na wale wa upinzani wazinduke na kuona ni ipi aina ya chama mmbadala ipatikane kabla ya kuweka mbele hamasa na jazba zinazopelekea nchi yetu izidi kuwa ya tano kutoka mwisho kwa masikini Uliwenguni...

Mfumo wa siasa uliopo unatoa fusra ya kufanya mabadiloko ya utawala ingawaje mabadilko yanazingwa na utata wa mazingira ya sheria katika katiba iliyopo,hii haiwezi pia kuwa kikwazo iwapo vyama vya upinzani vianaweza kujipanga katika mstari mnyoofu wa kujenga nguvu ya hoja badala ya hoja zenye ubabe,vishindo, matusi na makelele.

Tanzania inaweza sana kujifunza kutokana na mabadiloko yaliyotokea Kenya wakati umma ulipoichoka KANU na kukabidhi ridhaa ya kura kwa NARC,lakini kilichotokea yale yote ambayo NARC ilakuwa ikilalamika dhidi ya KANU ndiyo yanayoendelezwa na NARC na kudidimiza uchumi wa nchi na kukithiri kwa vitendo vya rushwa. Leo Mwenyekiti wa Chama cha KANU Uhuru Kenyatta anasema hadharani kuwa tatizo halikuwa KANU, tatizo na kansa kubwa katika Kenya na ndani ya KANU ilikuwa ni Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki, Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na kundi zima lililojiondoa KANU na kukimbilia NARC, lakini KANU kama KANU ni safi na ndiyo iliyoleta uhuru wa Kenya na ustawi wa amani tokea uhuru wa mwaka 1962.

Hapa ndipo tunapoweza kupata mshawasha na kufikiri huenda yakatokea ya nyingi nasaba hatimaye ukatupata mwingi msiba,lakini watanzania ni werevu kweli kweli chemsheni Bongo 2005 amueni kwa ridhaa yenu na utashi mnaokusudia kwa mizania iliyo sawa ili ile Bongo Mchicha ipatikane nasi tuondokane na umasikini.

CCM chama kinachotawala kikiweza kujibadili na kukubali kubadilika kama ambavyo awamu ya Rais Bewnjamin Mkapa ilivyoweza kufanya maajabu katika ustawi wa uchumi na ujenzi wa miundombinu ina nafasi ya kujiweka katika jangwa jeupe la matumaini ya kuongoza Taifa hili katika mhula mwingine ujao.

Rasilimali zetu ni hazina na utajiri wetu. Ni vipi zinufaishe mataifa mengine na kuiacha Tanzania katika ukiwa usiokwisha miaka na miaka,tunataka Bongo Mchicha yenye neema na maendeleo bila ya ahadi kubaki katika majukwa, kwenye ilani za uchaguzi na vijitabu vilivyoanishwa sera za vyama.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.