SIASA ZA KILIBERALI NCHINI

Na, Mwandishi wetu

Katika hotuba yake ya mwisho kwenye ukumbi wa Diaomnd Jubilee(August 16, 1990) -- kabla hajavua kofia yake ya u-enyekiti wa CCM ngazi ya taifa;Mwl. Julius Kambarage Nyerere alifanikiwa kuanika wazi uvundo na mapungufu ya chama tawala(CCM) na kuonya kuwa,"bila CCM imara taifa letu litayumba..."

Mwl. alikaliliwa akisema, "...Ukiacha matukio machache sana, viongozi wa CCM hawana tabia ya kujali shida za watu. Hatuna utaratibu wala tabia ya kusikiliza watu wenye shida za kweli na kujaribu kuwasaidia. Kama Viongozi wetu wote wa ngazi mbali mbali wangekuwa na taratibu na tabia ya kuwasaidia wananchi tusingefikishwa hapa tulipofikishwa... Wananchi wenye shida za kweli kweli hutapatapa mno siku hizi kutafuta msaada." --Mwisho wa kunukuu.

Ukweli wa mambo ni kwamba:Hali hiyo ya uvundo ndani ya CCM wenye lengo moja la kuwapuuza na kuwasahau 'walalahoi/wanyonge' walio wengi--bado unazidi kuvunda mpaka hivi leo licha ya Mh.Kikwete kusimama jukwaani [Bahi,Dodoma] juzi na kuanza kupinga waziwazi rekodi mbovu za chama tawala katika kipindi chote cha miaka 41 madarakani...

Tukianza na serikali ya awamu ya kwanza [Mwl. Julius Nyerere]:--Kidogo, vilio vya wanyonge wengi vilisikilizwa. Ila kutokana na mfumo mbaya wa siasa za kisoshalisti, matatizo mengi ya wanyonge hayakuweza kupatiwa ufumbuzi wake.

Usoshalisti--ni mfumo ambao CCM iliamua kuufuata katika kipindi ambacho dunia ilikuwa imegubikwa na vuguvugu kali la vita baridi;Ingawa wasomi mbalimbali waliobobea hususani katika maswala ya kiuchumi walimshauri Mwl kuwa mfumo huo haukuwa na manafuaa yoyote yale kwa taifa changa kama vile Tanzania...Mwl hakutaka hata kuwasikiliza. Matokeo yake-- nchi ikazama katika dimbwi kubwa la umasikini juu ya umasikini.

Basi,serikali hiyo ya CCM ikaenda zake ikapita huku ikishindwa kabisa kutatua matatizo lukuki ya wananchi walalahoi wa kitanzania. Kwanini?--kwasababu tu ya kung'ang'ania mfumo wa kisoshalisti ambao uliwafanya walalahoi wazidi kuwa masikini badala ya kuwakwamua toka katika janga hilo.

Baada ya hapo,ikaja serikali moja ya ajabu kabisa! Serikali ya Mzee Ruksa.Serikali ya awamu ya pili --chama ni CCM.

Mtawala wake akaibuka na kanuni ngeni kabisa za kiuchumi--'sera za ruksa' ambazo hazipatikani kabisa katika kamusi za kiuchumi.Ghafla, nidhamu ndani ya chama na serikali ikatoweka.Watu wachache wakajikusanyia vyao huku wakiwacha walalahoi wakiwa wameduwaa wasijue la kufanya. Maana yake ni kwamba--wakaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za "Sisi" na "Wao". Huku wakiacha watu wachache wawe na mali na nguvu, na fidhuli ya kuwa na mali na nguvu; na watu wengi wawe maskini na wanyonge.

Miaka kumi ya utawala huo mbovu wa serikali ya awamu pili ikapita.Na kwa mara nyingine tena chama tawala CCM kikarudi madarakani kuunda serikali ya awamu ya tatu.

Kwa upande wake,Rais Benjamini Mkapa alijitahidi sana kurejesha nidhamu ndani ya serikali. [Kwahilo--makofi tafadhali....];mianya mingi ya rushwa ilifugwa na serikali ikakusanya mapato mengi sana--nadhani kushida hata serikali mbili za awali (serikali ya awamu ya kwanza na ile ya pili.) kwa pamoja.

Lakini mbali na mapato yote hayo,walalahoi bado hawakunufaika kimaisha katika kiwango ambacho walistahili wanufaishwe.Tizama maliasili zote zilizopo nchini,lakini bado Tanzania imesalia katika nafasi ya tano kwa umasikini duniani tukipitwa na nchi nyingi zisizo na utajiri ambao Tanzania imejariwa. Mfano,mbuga za wanyama,mito,maziwa,madini,ardhi yenye rutuba...

Kinyume chake, sehemu kubwa ya mapato hayo yalitumika kulipa deni kubwa la kigeni ambalo hata kama walalahoi hao wangejifunga mikanda namna gani--wasingeweza kumalizia kulilipia. (nchi wahisani nao wanajua hilo).Tunashukuru kuwa deni hilo limefutwa chini ya juhudi za Blair.

Muda si mrefu ndugu wananchi,serikali ya awamu ya tatu itakuwa ni historia...Lakini kando ya hilo,kuna kila dalili kuwa chama tawala--CCM kinaweza kikarejea madarakani tena kwa awamu nyingine ya nne.

Na kuhakikisha kuwa hilo linatokea,safari hii CCM wameibuka na mbinu mpya kabisa!--Mbinu inayo wapumbaza wapinga kura walio wengi (vijana sana sana),pasipo wao kujua.

"...CCM imewapa vijana--kijana mwenzao ambaye ndiye dawa ya kichwa kinachowauma wote vijana..." Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi katika ukumbi wa Diamond Jubilee alisema kuwa vijana wana kila hali ya kujivunia kumpata mgombea ambaye ni kijana mwenzao na aliwaeleza dawa ya matatizo yao ipo kwa Kikwete. "...Msituangushe mfikisheni Ikulu, vijana ambizaneni na vijana wa CCM na vijana wa upinzani kwamba dawa ya kichwa imepatikana, vinginevyo wazee watawachekeni," alisema Mwinyi.

Hapana kwa Mzee Mwinyi! Hapana kwa Rais Mkapa! Hapana tena kwa viongozi wote wa CCM wanaowashawishi vijana wampigie Kikwete kura eti kwasababu tu yeye ni kijana mwenzao.

Ujana siyo sababu ya msingi ya kutosha kumpatia mtu dhamana ya kuongoza taifa lenye watu zaidi ya millioni 35--isipokuwa ni uadilifu na uwezo mzuri wa kutatua matatizo ya watu hao ndio unaohitajika.Miaka 41 ya nchi kunyonywa na 'kagenge' ka watu wa chache sasa basi!

Ujana tu,pasipo sera nzuri za kutatua matizo yanayowakabili vijana kwasasa usiwarubuni vijana wazalendo wa Tanzania.Vijana wanachohitaji kuambiwa ni sera na manifesto ya chama kuhusu jinsi gani ambavyo kitatatua matatizo ya sasa yanayowakabili vijana hususani swala la ajira na sio wimbo wa kila siku wa "Kikwete ni kijana mwenzenu..."

Kadhalika, Mh.Kikwete, ulikosea juzi mjini Dodoma [Bahi] kwa kudai kuwa ,"...wanaosema CCM haijaleta maendelo mubadala tangu Tanzania ipate uhuru wahana macho".Maana historia haiongopi!

Mungu Ibariki Tanzania

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.