BILA KUANGALIA HISTORIA YA ZANZIBAR, MUUNGANO NI NDOTO

Na, Antar Sangali,Bagamoyo

Zanzibari yaani Unguja na Pemba ni Taifa dogo lenye historia pana kuliko nchi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Na bila kuangalia Historia ya Zanzibar kiundani ni vigumu sana kukiunganisha kisiwa hicho kisiasa na kudumusha Muungano wa Tanzania uliodumu kwa miaka thelathini na mbili (32).

Historia ya Zanzibar kabla na baada ya kupita Mapinduzi ya mwaka 1964 unaweza kuita ni historia inayowahusisha majini na wanadamu katika jumla ya maisha na ustawi wa maendelo [yao] iwe kisiasa , kijamii na kidemokrasia. Na ikiwa unaweza kuanza katika kubaini kiini cha historia ya kweli bila shaka unaweza kuijua na kuitambua vema Zanzibari yaani Unguja na Pemba, watu wake, akhlaq zake , silka na viongozi wake waliopita, waliopo, na wanaopigania kushika utawala. Kiufupi, Zanzibar ilikuwa na makundi ya kijamii, kikabila, na kirangi tokea zama na zama kulingana na maisha ya watu wake na maendeleo yao siku baada ya siku.

Zanzibari [Unguja na Pemba] ni visiwa vilivyobeba hazina kubwa ya historia yenye mchanganyiko mkubwa wa damu katika vizazi vya jamii yao, na hilo si jambo linaloweza kubezwa na kupuuzwa unapojaribu kuzungumzia hali ya Muungano. Zanzibar hailingani japo thuluthi kihistoria na Tanganyika nchi ambayo imeungana na Zanzibar na kupatikana kwa Taifa la Tanzania April 26, 1964.

Mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanzishwa chini ya Sultan ukisimaiiwa na katiba ya Kiingereza, vyama vya siasa vilivyoanzishwa vilikuwa na sura ile ile ya makundi na hata kupelekea majina ya vyama hivyo kuwa na majina ya kikabila mathalan African Association (AA) na Afro Shiraz party (ASP). Joto la kisiasa lilipelekea kuanzishwa kwa vyama vingine baadaye vya Zanzibar National Pary (ZNP) Chama cha Kikomonisti cha Zanzibar, Zanzibar and Pemba People's Party (ZPPP) na UMMA.

Mfano, Chama cha ASP kilichoanzishwa mwaka 1957, ZNP 1955, ZPPP 1959 na UMMA 1963 wagombea wake walitokana na vyama vyao au Jumuiya za kidini na kikabila. Sher M. Chowdhiry alisimama kwa Muslim Association, Ibun Saleh alisimamishwa na Comoria Association na baadhi ya wagombea wengine walisimama kama wagombea binafsi mathalan Anverali Mukri, Abdullah Busaidy, Abdul Mukri na Haji Juma.

Katika uchaguzi Mkuu mwaka 1957 ASP kilichoongozwa na Abeid Aman Karume kilipata jumla ya kura 45,172 sawa na asilimia 50.6 , na ZNP cha Ali Mokhsin Al-Barwan kikapata 31,681 sawa na asilimia 35.5. Lakini katika mwaka 1961 ASP ilipata jumla ya kura 53,232, ZNP 26,572,na ZPPP cha Mohamed Shamte aliyejiengua toka ASP kilipata 4,57 .

Swali kubwa la msingi la kujiuliza ni kwaniniMapinduzi mwaka 1964 yalitokea licha ya ushindi waliopata ZPPP baada ya kuunganisha viti vyao na ZNP na kuunda serikali ili kupewa uhuru toka katika koloni la Kiingereza lililokuwa likilinda maslahi ya utawala wa Kisultan tokea mwaka 1890?

Kundi la wananchi waliokuwa weusi waliunganishwa pamoja na ASP katika kuhakikisha wanapata haki za kujitawala na ustawi wa kumiliki uchumi na njia kuu za uzalishaji mali na vitega uchumi ili kuondokana na Umwinyi na Ubwenyenye uliokuwa ukihodhiwa na kundi la waarabu na machotara.

Waafrika weusi hawakuhisi abadan kama walikuwa na haki katika visiwa hivyo na hivyo kuweka mkazo zaidi wa kuweza kupata madaraka ya utawala na hasa ukichukulia wakati huo vuguvugu la mabadiliko ya ukombozi duniani na hususan Barani Afrika kuanza mara bada ya kumalizika vita ya pili ya dunia.

ASP iliona madaraka ya utawala chini ya ZNP na ZPPP ni sawa na kubaki hisia zile zile za utawala wa Kiingereza na Kisultan katika Zanzibar na hivyo kulazimika kuandaa Mapinduzi yaliyomwaga damu za watu na hatimaye kupata nafasi ya kushika utawala uliowaunganisha wazanzibar wote katika umoja na maelewano mapya visiwani humo.

Mapinduzi ya ASP yalitimia kwa mchango mkubwa wa kundi la vijana wasomi na wanasiasa wa siasa za Lenin na Karl Max waliojiengua toka Umma Party wakiongozwa na Mjamaa Abdulrahman Babu hadi kufanikiwa kwa Mapinduzi hayo 1964.

Hasama, chokochoko na chimbachimba za kisiasa huku Wazanzibar wakizidi kuhitalafiana ilizidi kuchukua sura mbaya zaidi zikianzia ndani ya ASP yenyewe, wakaanza kunyoosheana vidole vya kutaka kupinduana na wengine kukamatwa na kufungwa magerezani katika mahakama za ‘kimapinduzi” ambazo hazikuwa na mifumo ya sheria ili kupima haki na wajibu kwa wafungwa.

Viongozi kadhaa waliokuwemo katika serikali ya kwanza ya Abeid Aman Karume walianza kuhitalafiana wakiwemo aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Kassim Abdula Hanga, na wengine akina Othman Shariff, Saleh Saadalah, Mdungi Ussi, Jaha Ubwa, Idrisa Majura na wengine kadhaa wakasehelea magerezani ambapo hakukuwa na mifumo ya sheria ili kupima haki na wajibu.

Mwaka 1964 yakapita mapendekezo ya kisisaa katika kujenga Muungano wa Taanzania na Zanzibari, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walikubalina katika mambo kumi na moja [eleven articles of Union] na masuala hayo yapitiwe na kutazamwa upya na pande zote mbili iwapo yanakidhi haja ifikapo mwaka 1974.

April 7, 1972 Rais wa kwanza wa Visiwa hivyo Karume alipigwa risasi na Luten Homoud Mohamed na kumpotezea maisha yake. Kundi kubwa la viongozi waliohusishwa na tuhuma walikamatwa ma wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Sheikh Aboud Jumbe akashika madaraka kurithi kiti cha Karume na ulipofika mwaka 1977 Jumbe alikubali rai ya Julius Nyerere ya kuunganisha vyama vyao vya ASP na TANU kwa maslahi ya mataifa yao na kujenga umoja zaidi wa kitaifa, CCM ikazaliwa. Lakini hili linatajwa na wasasisa wajuzi kama ulikuwa ni mpango wa kuikinga serikali ya Mapinduzi isipinduliwe tena na kundi lililopinduliwa mwaka 1963.

Jumbe na Nyerere walihitalafiana katika dhana nzima ya muundo wa Muungano. Ni wazi kwamba Jumbe hakuafiki utekelezaji wa makubaliano 11 ya Muungano uliosainiwa na Karume na Nyerere mwaka 1964 na kuamsha hoja ya kuwepo kwa serikali tatu. Mwalimu Nyerere msimamo wake ulikuwa ni serikali mbili kuelekea moja huku Jumbe na Waziri wake Kiongozi Ramadhan Haji Faki wakisisitiza 1+1=3 Nyerere akisema 1+1 siku zote ni = na 2.

Lakini Jumbe na Faki wakati wakiingia katika kikao cha Kamti Kuu ya CCM Taifa tayari nyaraka za hoja ya Jumbe zilikuwa mikononi mwa Nyerere alizopelekewa na Seif Shariff Hamad akimtuhumu Jumbe kuandaa kuvunja Muungano. Mtafaruku mkubwa ulizuka, mchafuko na hali mbaya ya hewa ya kisiasa ikatangazwa kuikumba Zanzibar na hatimaye Jumbe akalazimishwa kujiuzulu Dodoma bila ya ridhaa ya ASP ili kulinda maslahi ya umoja wa kitaifa na Muunagno wa Tanzania. Macho ya seif na kundi lake lililojiita Progressive la akina Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan likamezea mate na kuona huo ni wakati wao muafaka wa kukalia kiti cha utawala wa Zanzibar. Kinyume na matarajio yao kundi la Liberators la akina Abdalla Natepe, Nassor Moyo, Said Bavuai, Ahmed Ameir, Khamis Daruwesh na wengine wakaibaini dhamira hiyo ya vijana kukataa mgombea asitoke katika kundi hilo.

Kimsingi matumaini ya Seif Sharif Hamad baada ya kutupwa na Idris Abdul Wakili yalianza kuamsha upya mjadala ma mabishano makali ya kisiasa na ndipo kundi toka Pemba lilipoamka na kudai wapemba wanatengwa katika medani za Urais wa Visiwa hivyo. Kampeni za urais wa Wakili zilikumbwa na uzito na mzigo wote wa lawama akatupiwa Seif kwa kudhoofisha kampeni dhidi ya ushindi wa Wakili Pemba.

Hata hivyo kimsingi ipo semi iliyomea Visiwani humo kwamba wapemba hawatofaa kushika madaraka ya uatwala katika seriakali ya Mapinduzi Zanzibar, kwasababu hawakushiriki katika harakati za Mapinduzi na ZPPP ya Shamte ilikataa kuunganisha viti vyake na ASP ili kupata uhuru mwaka 1963.

Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM haikuridhishwa na hoja za akina Seif na kundi lake hasa za kuhoji masuala ya Muungano na hivyo maamuzi ya CCM yakawa ni heri wapinzani wao wakawa nje ya chama chao kuliko kubaki ndani ya chama hicho na kuendele kupingana kinyume na sera na msimamo wa CCM.

CCM iliwafukuza Seif na wenzake na hatimaye ikapelekea Waziri Kiongozi huyo wa zamani kuishia gerezani kwa kile kilichodaiwa baadaye kwamba alikutwa na nyaraka za siri za serikali na hivyo akabaki kizuizini kwa miaka mitatu hadi shauri lake lilipotupwa na mahakama ya rufaa Tanzania mwaka 1992.

Kufukuzwa kwa Seif na wenzake Dk Salmin Amour na Dk Salim Ahmed Salim waliona tayari mwanya kuirithi nafasi ya Wakili endapo muda wake wa kujiuzulu ukifikia jambo linalodaiwa yale mawazo ya ki-Progressive ya akina Salmin, Adam Mwakanjuki, Issack Sepetu na Salim na wengine yakafifia ghafla na kubadilisha mwelekeo.

Harakati za kudai mageuzi ya kisiasa zikaanza visiwani Zanzibar, Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Maulid Makame, Soud Yusuf Mgeni wakaunda Kamati Huru ya mageuzi ya kisiasa (KAMAHURU) kwa lengo la kuishinikiza SMZ ikubali mabadiliko ya kisiasa na kufuta mfumo wa chama kushika hatamu.

Kundi hili ni kundi lililotoka katika mikono ya CCM, baadhi yao ndiyo waliyomsaliti Jumbe katika kumuona ana lengo la kuvunja Muungano, ndilo kundi lililompiga vita Wakil asiwe Rais na kudai kuna ghiliba ya kura ndani ya CCM mpaka akawa Rais wa awamu ya nne Zanzibar.

Wazanzibar wanajiuliza iwapo matlaba na matarajio yao yangeweza kutimia ndani ya CCM kundi hili lingeweza kuthubutu kutoka CCM na kuanzisha mageuzi ya demokrasia?, Au ni baada ya kufukuzwa na kushindwa kuyafikia malengo walioyakusudia ya kushika madaraka ya utawala?

Moja kati ya madai ya CUF ambako kuna kundi kubwa la waliofukuzwa toka CCM ni kwamba CCM imevuruga matakwa ya Muungano toka masuala 11 hadi kufikia zaidi ya 24 kinyume na makubaliano, dai jingine mfumo unaofa sasa ni wa serikali tatu badala ya mbili ili kuipa nafasi pana Zanzibar kujiamulia mambo yake yenyewe.

Kila mzanzibar na Mtanganyika anafungua masiko na kujiuliza: je, hivi zile hoja za Jumbe za kutaka serikali tatu sasa zimetekwa nyara na CUF? Hivi Jumbe alitoswa kiroho mbaya tu ili asiwe kikwazo cha watu kufikia matlaba na dhamira zao? Hivi ni kweli kwamba hili kundi [CUF] linalilia maslahi na kuwaunganisha wazanzibar au ni kundi linalopigania kupata madaraka baada ya kushindwa kuyapata wakiwa ndani ya CCM?

CCM inashikilia kutaka kudumisha Mapinduzi daima ya kihistoria,huku CUF inapigania na kuhakikisha uhuru uliopatikana 1963 chini ya uchaguzi uliokuwa huru na haki unaheshimiwa na kusema Mapinduzi yabaki kuwa ni historia huku wakituhumu chini ya kauli mbiu ya Mapinduzi Daima hayapatikani mazingira ya demokrasia hususan ya uchaguzi huru na haki.

CCM chini ya SMZ na SMT wanahimiza kuwa asiyethamini Mapinduzi ni msaliti na hafai japo kupewa madaraka ya Mtaa huko Zanzibar kwasababu Mapinduzi hayo ndiyo yaliyoondoa ubwama na utwana, kujenga ustawi sawia, na pia kuleta heshima kwa wazalendo wa nchi hiyo. Hayo tumeyasikia sana kila tunapokuwa tunakaribia kuelekea kwenye uchaguzi mkuu huko Visiwani. CCM inadai hadharani kuwa wapinzani hawa wa leo [Visiwani] ni wale wale waliopokonywa madaraka na ASP mwaka 1964. lakini CUF inasema haina minasaba na vyama vyote vya kizamani yaani ASP, ZNP, UMMA wala ZPPP. Je? Makundi haya mawili ni makundi yanayotazama maslahi ya nchi au yanagombania madaraka ya utawala kwa manufaa yao binafsi? Je, maneno ya Mwalimu ya kuunda seriakali ya umoja wa kitaifa huko visiwani yana nafasi kweli leo hii!?

Ni jambo la busara kutazama historia ya kisiasa huko Visiwani tukianzia enzi za ukoloni hadi leo na kisha kulinganisha na matokeo ya chaguzi zote zilizowahi kufanyaika huko ili kujua ni kwanini chaguzi hizo zimeamuriwa kwa idadi ndogo tu ya kura.

Na ingawa CCM nayo haiko radhi kuona inapoteza historia yake azizi ya kupigania Mapinduzi ya 1964, Zanzibari inahitaji viongozi na watu wake kuvumiliana, kustahamiliana, kushirikiana na ikiwezekana kuunda serikali ya pamoja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010. Hili ni muhimu kwasababu CUF ikishindwa uchaguzi ujao itadai imeibiwa kura. Imedai hayo mwaka 1995, 2000 na 2005. Zanzibar inahitaji kutazamwa kwa macho ya huruma maana kuvurugika kwa amani visiwani humo ni mzigo mkubwa kwa upande wa Bara. Vilevile, wananchi wa Visiwani wasisahu kuwa bila ya kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, amani na utulivu Visiwani humo ni ndoto. Maelewano ya Mpemba na Muunguja yaliyopo hivi sasa yatatokomea kama moshi ikiwa Muungano utakufa leo hii.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.