KIKWETE NA TURUFU VIGANJANI

Na, Antar Sangali,Bagamoyo

Jakaya Mrisho Kikwete ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Tanzania ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Waziri kamili wa Nishati na Madini na baadaye Waziri wa Fedha.Mh.Jakaya ni kada na Mwanasiasa aliyelelewa na kubebwa katika mbeleko na mikono ya vyama vilivyoleta Uhuru na Mapinduzi yaani TANU na ASP.

Ni mtu au kiongozi aliye na mvuto na ushawishi mkubwa katika medani za siasa na kubahatika pia kukomaa katika viunga vya diplomasia kwa takriban miaka isiyopungua kumi chini ya Rais anayemaliza muda wake nchini Tanzainia.

Kikwete aidha ana chumo jingine au amepata uzoefu mwingine wa ziada katika kushiriki kwake kwenye vikao vya upatanishi wa migogoro ya kisiasa na kivita nchini Burundi hadi kufikia suluhu iliyo na angalau machoni.

Jina la Kikwete lilianza kupata mng'ao ulioleta matumaini kwake mwaka 1995 pale alipojikita na kutupa mshipi katika mbio za kuwania urais akiwa jopo la zaidi ya watu 17 kupitia Chama Cha Mapinduzi.Lakini Rais Benjamin William Mkapa kura zake zikatosha na kuwa mgombea wa CCM wa Jamhuri ya Muungano Tanzania mwaka huo.Kikwete na Wazuri Mkuu wa zamani Bw Cleopa Msuya kura zao kwa wakati ule hazikutosha.

Kikwete, Bw Prince Bagenda, Bw Jenerali Twaha Ulimwengu, Bw Edward Lowasa, Marehemu Mashaka Nindi Chimoto, Bw Seif Sharif Hamad, Bw Ami Mpungwe na wengine ni zao la TANU na siasa zake za Ujama na Kujitegemea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wakibukua na kutafuta Digrii zao.

Ni mirija iliyopitisha siasa za Mwalimu Julius Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ni makada walioshirikiana na Mtawala huyo kwa ukaribu, na Mwalimu aliwachukulia kama askari wake wa miamvuli kwa nyakati hizo licha ya kuhitalafiana na baadhi yao kulinga na wakati ulivyo katika maisha ya siasa.

Aidha Mwalimu Nyerere alijivunia sana kundi hili lilokuwa na vijana waliokuwa na upeo na hasa katika na kufuzu kwa siasa zake ndani ya Chuo Kikuu , ndani ya umma wa watanzania na pengine Afrika na dunia kwa upana wake.

Uhodari na ushupavu wa Kikwete ulianza kuonekana mapema toka akiwa ndani ya TANU na badaye CCM, kupenda kwake kujichanganya na watu wa aina mbalimbali ilikuwa ni silaha yake kuu vitani na pengine kufika kwake mahali hapa alipo leo nidhahiri atakuwa amevushwa na merikebu hii tunayoibatiza jina la ' Mv kujichanganya' .

Duru za kisiasa zinabaini kuwa,Kikwete alikuwa na mambo matatu ambayo pengine hata wapambe na masahibu zake wa karibu hawakuigundua siri hii iliyojificha ambayo ni ushupavu na ulimi wenye ufasaha, moyo wa stahamala, na uvumilivu na akili zenye ugumu wa kutokata tamaa mapema.

Uvumilivu wake ulidhihirika bayana mwaka 1995 pale kura zake zilipodaiwa kutotosha ndani ya CCM kule Chimwaga Dodoma na Rais Mkapa akatangazwa kuwa mgombea, ushupavu na ufasaha katika ulimi wake ulibainika pale aliposimama mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM na kutamka kinagaubaga kwamba anayakubali matokeo na kusema anavunja kambi yake ili kumpa nguvu Rais Mkapa, lakini stahamala na uvumilivu wake ni matunda yaliyomfikia mwaka 2005 aliposhinda kwa kishindo ndani ya chama chake na kuwatupa mbali wenziwe akina Dk Salim Ahmed Salim na Prefesa Mark Mwandosya.

Akili na ugumu alionao wa kutokata tamaa mapema pengine huenda ukawa ni kafara la kumfikisha na kubisha hodi katika milango ya Ikulu ya Tanzania. Siri hii sijui kama rafiki zake akina Lowasa, Abdulrahman Kinana, Ukiwaona Ditopile, Rostom Aziz,Stephen Wasira pengine hata mdogo wake Yusuf Kikwete na wengine kama waliweza kuibaini mwanzoni, lakini kimsingi ana ushujaa na ushupavu unoaminika, stahamala iliyopevuka na ufasaha katika ulimi wake kupitia lahja yeyote ya lugha anazozitumia ama iwe ni Kikwere, Kiswahili na Kiingereza.

Akiwa Waziri wa Fedha mwaka 1995 kwa kipindi cha miezi sita "Mpiganaji huyu" aliweza kuwawajibisha Maafisa kadhaa katika wizara hiyo kufuatia utoaji wa misamaha holela ya kodi iliyotolewa kwa baadhi ya wafanyabishara na kulipotezea Taifa mapato.Sawa na Rais wa awamu ya pili katika Jamhuri ya Muungano Tanzania --Mzee Ali Hassan Mwinyi alivyomuwajibisha kwa manufaa ya umma aliyekuwa Waziri katika wizara hiyo Marehemu Profesa Kighoma Ali Malima.

Akiwa katika Wizara hiyo Kikwete aliweza kuunda au kufanya ubunifu wa mfumo wa chombo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) ambao umeweza kusaidia sana katika awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa kuweza kukusanya mapato toka Bilion 25 hadi kufikia Bilion 160 kwa mwezi. Lakini itakumbukwa vile vile akiwa Waziri wa Fedha jinsi alivyoweza kutengeneza bajeti iliyoweza kusifiwa na Bunge na ambayo kwa namna kubwa ilikuwa na unafuu na ilivyoweza kuigusa jamii hususani wakulima walioko vijijini na wafanyakazi serikalini ili kuweza kupata masurufu yenye tija baada ya kustaafu kwao.

Akiwa Waziri wa Madini na Nishati Kikwete uchunguzi unaonyesha alimudu vema kuweka sera mwanana iliyolazimisha watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa kuweka Benki dhahabu ,Tanzanite na almasi na kuwezesha kuinuka kwa mapato ya serikali na ustawi wa uchumi na kulinda kuanguka kwa thamani ya shilingi yetu.

Juhudi nyingine za Kikwete akiwa katika Wizara ya Fedha aliweza kusaidia kutafuta fedha ili kufanikisha uanzishwaji wa miradi ya maji katika Mji Mkuu wetu Dodoma na kumalizia tatizo kama hilo katika Mardi wa Wami-Chalinze uliogaharimu shilingi za Kitanzania Bilion 15 ambao ulijengwa kwa ufadhili wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Mwaka 1992 Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa joto na vuguvugu la piga nikupige na kurushiana makombora ya kisiasa kati ya Chama Tawala na kambi ya upinzania ulianza kwa mwendo wa haraka.Lakini kalenda ya Kikwete inaonyesha kuwa ana siasa za kati ambazo huwezi kuziweka katika mstari mnyoofu wa Mchungaji Chrostopher Mtikila na Dk Salmin Amour "Kamandoo".

Mwaka 1995 Tanzania ilifanya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa baada ya kupigwa marufuku mwaka 1965 na serikali ya TANU na kufa kwa vyama kama vile ANC, AMNUT na UTP.Uchaguzi huo kwa Tanzania Bara haukuleta na kuzua mtafaruku, lakini kwa Visiwani hali haikuwa shwari kwani chama cha pinzani cha CUF kilidai mgombea wake wa nafasi ya urais Seif Sharif Hamad ailiibiwa kura zake na kutangazwa Dk Salmin.

Ulipomalizika uchaguzi huo, CUF haikufyata mkia ilihaha ulimwengu mzima na kuishawishi Jamii ya Kiamatifa na nchu wahusani kuamini kuwa haki haikutendeka Zanzibar, na kilichofuatia ni chama hicho kutomtambua Dk Salmini kama si Rais halali na wajumbe wake wa Baraza la Wawakilishi kususia vikao na wanapoingia kukataa kuchangia hoja Barazani.

Kwa hakika ulikuwa ni mzozo mkubwa ulioigubika dunia na Tanzania nzima na pengine ulimkosesha raha sana Rais Mkapa katika ingwe yake ya wali kwenye utawala wake hatimaye kadhia hiyo ikaingiliwa kati na Jumuiya ya Madola chi ya Katibu Mkuu wake Chief Emeka Anyaoku na Mjumbe Maalum Dk Moses Anaf.

Lakini kabla ya kuingilia kati kwa Jumuiya ya Madola serikali zote yaani SMT na SMZ ziliziba midomo na masikio na kukaataa kila wakati kwamba hakukuwa na mgogoro wa kisiasa Zanzibar na uchaguzi 1995 ulikuwa huru na wa haki.

Kikwete akiwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa SMT mwaka 1995 mara baada ya uchaguzi huo alizitembelea nchi kadhaa za ulaya na Amerika katika ziara za kikawida za kiserikali.Katika mizunguuko yake alikumbana na kadhia ya kuulizwa maswali katika kila Taifa alilokanyaga kuhusiana na hali ya Zanzibar baada ya uchaguzi wa 1995.

Aliporejea nchini aliweza kuitisha mkutano na wandishi wa Habari katika Ofisi za Wizara yake na kutoa msimamo ulioleta mtikisiko na mshituko mkubwa katika masikio na macho hasa ya viongozi wenzake wa CCM wa Bara na Zanzibar pale alipodiriki kusema "...Zanzibar kuna mgogoro wa kisiasa na nisingependa Rais wangu aamini kuwa hakuna mgogoro huo Zanzibar, tunahaki ya kuushughulikia na kuutatua kwa maslahi ya nchi zetu."

Kuna habari za kutosha kwamba alithubutu kujenga hoja na ushawishi ndani ya chama chake ili kuafiki na kukubali kuandaa mazingira ya kumaliza tofauti zilizoko kufuatia kuzuka kwa mtafaruku wa kisiasa hatimaye kusainiwa kwa mara ya kwanza tarehe 9.6.1999 mjini Unguja katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kimsingi haya yalikuwa ni maneno toka katika kinywa chenye ulimi wenye ufasaha, kifua chenye ushupavu na ushujaa na ubongo wa akili ulioshiba stahamala na uvumilivu wa kutohofu kudhihirika ukweli na kupuuzia majuto yeyote yatokanayo na msimamo ulio uthabiti moyoni.

Kauli hii ilikuwa kama mithili ya hamira ndani ya beseni lililo na ngano na kujazwa maji,lilianza kuumuka kwa ghafla kwani Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere akawa mtu wa pili kushadidia kauli ya Kikwete na kutamka hadharani kwamba mgogoro unarindima Zanzibar. Mwalimu tayari alishabashiri na kutaka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi Zanizbar akiwa katika moja ya mkutano wa kampeni Mkoani Ruvuma pale mjini Sogea.

Kikwete katika kuonyesha ushupavu na ushujaa wa moyo wake na kujiamini alikuwa ni mmoja kati ya wagombea waliomuonyesha kidole hadharani aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM mwaka 1995 Dk Lawranmce Gama na kumwambia bayana na kupitia vyombo vya habari kuwa "Dk Gama anamhujumu" katika kampeni zake na Dk Gama mwenyewe hakusika kubisha au la kulalamika.

Kikwete miaka miwili kabla ya msimu wa kutaja dhamira za kuwania urais alikuwa akiamdamwa mno na vyombo vya habari ili avunje ukimya iwapo anatamaa ya kuwaniaa kiti kitakachoachwa na Rais Mkapa lakini msimamo wake ulibaki na ukawa ni kauli yake "...wakati wa kulizungumza hilo haujawadia ,tumpe ushirikiano Mhe Mkapa katika kujenga nchi na maendeleo ya uchumi."

Kikwete akiongozana na Mzee Peter Kisumo,Mkewe Salma Kikwete na Mdogo wake Yusuf kikwete aliitisha mkutano na wandishi wa habari katika ofisi za CCM Mkoa wa Pwani huku akiwa na karatasi za hotuba aliyoiandika kwa ufundi mkubwa kisiasa lakini ndani karatasi hizo kukiwa na turufu iliyojificha ya ari, nguvu na kasi mpya,--'Tanzania yenye neema inawezekana.'

Hotuba ilijaa pambio ,kuwekewa mizania, vibwagizo,mbinu na nahau zilizotimia katika uwanja wa siasa na utwala wenye matumaini mbele ya watanzania.Akaainisha namna bora ya serikali aitakayo katika dhana nzima ya uwajibikaji, utumishi unaofaa, kufanya kazi kwa bidii, kupiga vita Rushwa, matumizi bora ya rasilimali zetu, ubadhirifu na wizi serikalini, matumizi endelevu ya ardhi,uvuvi, ufugaji na kilimo cha kisasa na mambo kadhaa ya kutumai.

Pale pale wataalamu wa mambo ya siasa [ siku ile ile ] wakabaini kuwa; endapo hatopatikana mgombea mwingine mweledi na mjuzi wa mbinu aidha ndani ya CCM au nje na kisha kushindwa kuramba turufu piku katika jozi ya karata, turufu hii ya ari, nguvu na kasi mpya ni lazima itawatoa mrisi mahasimu wake.Ni kali, inatisha, inahamasisha, inamvuto na imebebeshwa ladha na uzito unaostahili.

Watazania wengi wameonekana kumtazama Kikwete katika macho ya matumaini na penginekulingana na ukubwa wa Chama Chake na hasa mizizi iliyojichimbia chama hicho tokea mwa 1954 kuanzia TANU na tokea mwaka 1957 ilikotokea ASP na bila shaka pengine kikapata ushindi mwaka 2005.

Mgombea huyo anaonekana kuwashawishi watu wengi kutokana na ile tabia yake ya kujichanganya na kuonekana rafiki wa kila mtu, ucheshi alionao, lakini kuna kundi la wasomi, watumishi serikalini, wafanyabiashara na wataalam mbalimbali ni kinachoonekana kuwapa mvuto na imani watu hao wengi ni matendo ya Kikwete mbele ya umma kama Kikwete na si CCM kwa asiilimia nyingi kama Chama cha siasa anachotoka na kumpa tiketi.

Anahukumiwa kutokana kwa umakini alionao, kuwajibika kwake, umahiri na historia yake kisiasa, kuwatumikia watu, kuwasaidia,heshima, kujua na kuheshimu mipaka ya utatwala, kumudu uvumilivu na katika mazingira ya kisiasa hususan za vyama vingi, lakini kubwa hapendi masikhara na mchezo katika kupanga na kusimamia majukumu yanayohusu maendelo ya watu.

Dhamana hii aliyoitaka Kikwete ni nzito nchini kwetu ,mizani ya kumpima na kuona anatosha vipi kuibeba ni kutokana na mambo kadhaa aliyoyafanya akiwa serikalini kwa miaka 17, kusimamia, kutekeleza, kutafuta kwa njia za ushawishi wa kidiplomasia na kuwa hodari katika kubuni mbinu na sera zenye mwelekeo.

Kikwete ana dhamna kubwa ya kuwatazama watanzania nakuwapatia wanaachokihitaji na si kutanguliza mbele matakwa na maslahi ya CCM au kujiongezea umaarufu huku wananachi wakiendelea kuishi katika dimbwi la umasaikini,wakikabiliwa na magonjwa, huduma duni za afya,ujinga na unyonge ndani ya nchi yao yenye rasilimali chekwaa!!!!. Macho ya watanzania wote Bara na Visiwani yanamtazama Kikwete kwa umakini, uangalifu na ustadi mkubwa hatua baada ya hatua ili kubaini vipi atazicharanga karata huku akiwa na turufu zake za ari,nguvu na kasi mpya.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.