MPATIENI RAIS BUNGE IMARA

Na, Antar Sangali, Bagamoyo

Lau kama safari hii tena wangepatikana wabunge wa upinzani kama wa mwaka 1995/2000, Mh. "JK" angepata nguvu nzuri ya kumsaidia kujenga Tanzania lenye neema tunayoitaka, kama tuiitavyo--"Bongo Mchicha". Sote tunalikumbuka lile Bunge la upinzani la mwaka 1995 la kambi ya upinzani lilivyokuwa moto katika hatua zake za mwanzo kabisa.

Wakipatika wabunge wengi na hodari wa upinzani safari hii tena, Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania litawaka moto na kuifanya serikali ijayo kuwa makini na mahiri zaidi katika utendaji na ufanisi utakaotukuka na pengine kukumbukwa katika kurasa za historia ya Bongo yetu.

Bunge la mwaka 1995/200 ni Bunge lililoleta matumaini na kuifanya nchi yetu kuonyesha uvumulivu katika uwanja wa siasa, matumizi ya nguvu ya hoja Bungeni na ukomavu mkubwa katika dhana nyingine mpya ya ujenzi wa nchi kisiasa, kijamii na kimaendelo.

Laiti kama itapatikana ile safu ya akina Bw. Mabere Marando, Bw. Masumbuko Lamwai, Bw. James Mbatia, Bw. Makidara Mosi, Bibi Fatma Maghimbi, Bw Ndimara Tegambwage, Bibi Naila Majid, Bw Augustine Mrema, Bw. John Cheyo, Bw Danny Makanga, Bw. Issack Cheyo, Bibi Chiku Abwao, Bw. Aman Kaborou, na Bibi Edith Munuo ni hakika ingemsaidia Kikwete kuivuta na kuileta ile Tanzania iliyo mbali na watu wake miaka mingi sasa tangu itambuliwe kuwa Jamhuri huru.

Lilikuwa ni Bunge lililoleta shauku na hamu kwa wananchi kupenda kulisikiliza, kusoma magazeti na kutazama vipindi vya televisheni kutokana na utoaji na uwasilishaji mwanana wa nguvu ya hoja uliokuwa na werevu na weledi katika kuchangia, kukubaliana na kupingana pale ilipobidi.

Bunge lile kwa namna kubwa liliisaidia sana serikali ya Rais Benjamin Mkapa kujipanga na kufanya maajabu ambayo leo watanzania waliokuwa nje kwa miaka 20 watakapo kuja-rejea nchini wataamini Bongo inaelekea katika kuwa mchicha kutokana na mabadiliko ya kiuchumi hali kadhalika maendeleo makubwa ya kipepari tuliofikia kuliko yale tulioyoyazoea ya kujenga ujamaa na kujitegemea, ambayo nayo yametuwezesha kujenga umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu, amani na utulivu madhubuti na kupenda kuhurumiana.

Bunge lile lilikuwa imara na madhubuti kwa namna iliyokuwa na taswira njema katika mustakabali wa nchi yetu, liliisukuma serikali na kuielekeza pale penye kasoro na urasimu, ni Bunge ambalo halikupenda kusinzia na kupiga soga au kusubiri tu posho ya vikao.

Bunge la upinzani la mwaka 1995/2000 lilitaka kutetetreka pale lilipotaka kugeuzwa ni jukwa la kisiasa na Bw. Mrema na hasa pale alipoibua hoja dhaifu akidai serikali ya CCM inaandaa njama ya kumuua yeye Mrema na Bw. Seif Sharif Hamad kabla ya mwaka 2000 na kusema anao ushahidi. Bunge lilipomtaka Bw. Mrema kupeleka ushahidi wake cha ajabu akapeleka Cutting za magazeti na kushindwa kukidhi nguvu ya hoja yake na hatimaye alipotakiwa kujitetea Bungeni akasena aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu na hata alipokuwa akienda Dodoma siku hiyo hakujua kama angekutwa na mkasa huo.

Itakumbuka kuwa wabunge kadhaa akina John Masilingi, Marehemu Balozi Ahmed Hassan Diria, Bw James Mbatia, Bw Mabere Marando Masumbuko Lamwai na Bw. Feredrick Sumaye walimshambulia sana na kumwambia amezoea kuzua. Hapa kidogo kutokana na tukio hili Bunge katika kambi ya upinzani lilitaka kupoteza ile ladha yake asilia iliyokuwa ikiwapendezesha wananchi wengi kupenda kulisikiliza Bunge na kulifuatilia hatua kwa hatua.

Chama Cha Mapinduzi -CCM- kinahimiza kwa wanachama na mashabiki wake kutimia kwa dhana ya kujenga mafiga matatu mwaka 2005 yaani Rais, Mbunge, na Diwani watoke CCM kwa minajili ya chungu kichemke katika mfumo wa kuwasha kuni zinazowaka kwa nguvu, ari, na kwa kasi mpya na labda kiwe kinapika kwa umakini na uthabiti

Ni kweli kisiasa kila chama kinahitaji kuwa na nguvu ya kutawala aidha katika serikali, Bungeni na kwenye halmashauri za wilaya, manispaa na miji ili kupitisha mikakati yake bila ya kupata ushindani na kupingwa. Lakini dhana hii tukiitazama katika wakati uliopo haina tofauti na ule wakati alioutaja Shaaban wa Robert katika kitabu chake cha KUFIKIRIKA pale alipoandika kwamba kabla ya elimu haujatambulika; Mvi zilihesabiwa kama alama ya hekima na busara, lakini akasema wakati huo umepita na wala hautorudi tena mtu asipoelimishwa hawezi kuelimika.

Maneno haya ya Shaaban Robert katika nchi ya kufikirika ambayo yalitoka katika kinywa cha Karama mtu aliyetaka na kulilia mbele ya miliki ya Mfalme wa nchi ile kuwepo na kuanzishwe kwa utawala wa sheria, yanafanana sana na Bunge lile la kambi ya upinzani mwaka 1995/2000 siyo hili la 2000/2005.

Bunge la 2000/2005 lilikuwa doro, rojorojo na halikuichemsha serikali kama ambavyo Bunge lililopita la mwaka 1995/2000 lilivyochachafya na kuwa na watu wenye upeo katika kujenga nguvu ya hoja na kuisugua serikali kwa maana ya kujenga nchi.

Zama na wakati wa kusema nchi yetu Tanzania itajengwa na upande mmoja wa aina ya watu au chama fulani cha siasa zimepita kama ambavyo mvi leo hii si alama tena ya hekima na busara kuliko elimu na mtu aliyeelimishwa na kuelimika.

Historia ya vyama vya TANU na ASP ni ndefu na ni vyama vilivyowekeza katika maisha ya watanzania na wazanzibar,cvina muundo wa chama cha kisiasa ambao umeanza katika miaka mingi dahari na baadaye kutandaa katika Bara zima la Afrika.

CCM kuiondoa katika madarakani kwa mwendo wa haraka kunahitajika kazi ya ziada na ni lazima kwa namna iliyo kubwa mpaka maneno ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yatimie kwa ile kauli yake kwamba "upinzani wa kweli wa kuiondoa CCM utatoka ndani ya CCM."

Kupambana na CCM kunahitajika kupatikane kundi la watu wenye amana na kuaminika katika jamii ya watanzania na ambalo ni safi kuliko kundi lilolomo sasa katika kushika na kuongoza utawala ambao unalalamikiwa na wananchi walio wengi. Kundi lililo katika kambi ya upinzani bado halijawa na mvuto wenye haiba ya kuweza kuwekeza na na kuishawishi jamii ikubali kweli CCM imefika mahali haitakiwi na haifai kutokana na jinsi CCM yenyewe inavyoweza kujibadili na kufuatana na wakati ulivyo.

Kundi la upinzani limejigawa katika makundi mengi yanayokosesha umoja wenye nguvu na kukomaa kwa vyama vyao jambo ambalo kwa namna kubwa linaifanya CCM izidi kujiimarisha na kufanya zoezi zima la kuing'oa kwa kazi ngumu kila kunapokucha.

Mfano, ingelikuwa vema watu kama akina Profisa Leonard Shayo wa Demokrasia Makini, Profisa Ibrahim Lipumba, Bw. Juma Duni (CUF), Bw. John Cheyo, Bw. James Mbatia, Bw. Polisya Maiseje, Bw. Josheph Selasini Dk. Senkondo Mvungi, Bw. Mosena Nyambabe na Bi. Naila Majid Jidawi wa NCCR-Mageuzi na Mchungaji Christopher Mtikila wa DP. Wengine akina Bw. Freeman Mbowe, Bw. Shaibu Akwilombe, Bw. Anthoy Komu, Bw. Zitto Kabwe, Bw. Jumbe Rajab Jumbe wa Chadema na Bw. Aman Nzugile Jidula Mabambas wa CUF wangelikuwa na shabaha ya kutaka kuingia Bungeni na kufanikiwa, ni wazi kungelikuwa na ari katika bunge la 2005/2010 na watanzania wangeweza kuingiwa na matumaini.

Lakini cha kushangaza wengi kati ya hawa waliotajwa wanataka Urais kwa njia ya mkato huku vyama vyao vikiwa havina matandao wa kutosha katika nchi (i.e. oganaizesheni hafifu isiyo na utimilifu wenye takwimu, sambamba na uhaba wa makada wenye uwezo wa mdogo wa kunadi yale wanayoyakusudia na kuyaeneza kwa maana ya sera zao namuonekano imara wa umoja wao).

Bunge la mwaka 1995/2000 lilimsaidia sana Rais Mkapa kuijenga nchi Tanzania katika sura ya Bongo Mchicha tuitakayo katika mustakabali mwema machoni mwa watu wa nje na ndani.

Ama kwa lugha nyinge nyepesi unaweza kusena Bunge lile lilimsaidia Mhe Rais kujipanga na kutekeleza yote chini ya falsafa yake ya uwazi na ukweli kwa mwendo wa haraka wenye usahihi.

Bongo ya leo si ile ya miaka thelathini iliyopita katika zile zama za kusubiri dona katika misururu mirefu ya foleni kwenye maduka ya ushirika, madarasa mabovu na zahanati zisizo na dawa lau Asprin au ile Bongo iliyokuwa watu wake wanaovaa vitambaa vya aina ya mpira na viatu vya matairi ya gari.

Rais Mkapa anaweza kutajika katika kumbukumbu za historia ya Tanzania iliyojaa neema baada ya kusota kwa miaka mingi na ushee kabla ya kupitishwa kwa Azimio la Zanzibar lililolizika Azimio la Arusha na kuufifisha mfumo na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa asilimia kubwa.

Ni wazi yamepatikana mageuzi na maendeleo ya kibepari katika nchi ya Tanzania, na laiti hali hii ikiweza kusambaa kwa kasi katika maeneo ya vijijini na kuimarishwa kwa miundombinu na kuwawezesha wananachi katika kumiliki na kuhodhi uchumi wao kitendawili cha kukaliwa na umasikini kinaweza kuteguka.

Kilimo kikiimarishwa na kuboreshwa ili kuwa cha kisasa chenye utaalam, pembejeo na matumizi ya mbolea, vyama vya ushirika vikitafutiwa masoko kwa ajili ya kuuza mazao yao, vijana wakiwezeshwa kupatiwa mitaji na taaluma ya kuwasaidia kusukuma maisha yao huku wanawake wakipatiwa fursa zaidi katika kumiliki mali na kupinga ubaguzi wa kijinsia ni wazi Tanzania na ile Bongo mchicha inawezekana.

Likipatikana Bunge toka kambi ya upinzani lenye watu madhubuti na wachapakazi litamsaidia sana Mh. Jakaya Kikwete kuijenga nchi katika kasi isiyo ya kawaida.

Hivi karibuni Mh. Kikwete alinukuliwa katika vyombo vya Habari vya Tanzania katika moja ya mikutano yake ya kampeni akiwa katika Mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu akisema kwamba asingelipenda kupata Bunge alilloliita Bunge au Mbunge "Ndiyo Mzee".

Kauli hii ya Mh. Kikwete kwa namna kubwa ndiyo inayomgusa kila Mtanzania na mpenda maendeleo na kuwafanya baadhi ya wananchi mfano, Jimbo la Tarime kushikamana na kuwa kitu kimoja katika harakati za kutaka kumg'oa kila anayesimama kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM na kutaka kchuagua upinzani/Chadema.

BongoTz hailengi abadan kuipigia upatu kambi ya upinzani ili kupata viti Bungeni dhidi ya CCM, lakini inawapigia mbiu na shime watanzania kuweza kukaa na kuamua kwa umakini hatima ya maendelo ya nchi yao.

Hebu watazame akina Mkwawa, Kinjekitile, Mirambo, Kimweri, Mangi, Meli, na Isike walilipigania Taifa na kupinga utawala wa Wajerumani na Waarabu si kwa kujitazama wao peke yao bali walilitazama na kulithamini Taifa lao na vizazi vijavyo. Juhudi hizi nidhahiri hazikutoka upande mmoja wa nchi na katika kundi moja au katika aina fulani ya mafiga, bali ni juhudi na jitihadi zilizoweza kuletwa katika matandao wa aina moja unaofanana katika kuihami nchi na kuinusuru na hatimaye sisi leo tunaringia matunda haya.

Wakati ambapo wanasiasa na vyama vya siasa hivi sasa wakiitazama dhamira ya kushinda viti vya Urais, ubunge na udiwani, sisi "BongoTz" hatuna chama lakini kwa kutumia turufu yetu ya utanzania tunapenda sana lipatikane Bunge la upinzani lenye watu makini na madhubuti ili liisaidia serikali ya Mh .Jakaya Kikwete kujenga "Bongo Mchicha" tunayoitamani.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.