KANZU MPYA, SHEIKH YULE YULE...

Na, mwandishi wetu

Katika duru za siasa za Kimataifa kuna vithibitisho kadhaa kwamba maraisi vijana hufanya vizuri. Mfano mzuri ni Marekani ambapo mwaka 1960 walipata raisi mpya kijana tu, bwana Kennedy na alikuja madarakani na nishati kubwa sana akiwaahidi wananchi wake mambo ambayo hayakuwahi kuingia akilini mwao kabla ya hapo.

Sambamba na bwana Kikwete, Kennedy na yeye alikuwa na sifa ya uzuri pamoja na mkewe Jacquiline, kama ambavyo Mama mkubwa mtarajiwa na yeye alivyo. Bahati mbaya Raisi Kennedy akauawa na kwa wengi wa wamarekani, ndoto ya maendeleo makubwa na kisiasa, kimaendeleo, kiutamaduni na utawala bora, vilikufa na raisi Kennedy. Ingawa nyingi ya ahadi za hali ya juu alizowaahidi zilitimia, ila hata sasa mambo yote yale ambayo wanadhani hayaendi vizuri au wagetamani yawe bora zaidi, wanaamini kama raisi Kennedy angemaliza muda wake, yangekuwa hivyo walivyotaka.

Hata katika miaka ya hivi karibuni raisi Clinton, na yeye kijana, na yeye mzuri, alifanya maajabu makubwa kiuchumi na maendeleo ya kijamii kwa Marekani kiasi kwamba ingawa alikuwa na matatizo mengi ya kimaadili, lakini bado watu wake waliendelea kumpenda sana na hata sasa wanasema kama isingekuwa uraisi unakoma baada ya vipindi viwili, angeweza kuchaguliwa tena kwa kipindi cha tatu kama angegombea.

Najua wengi mtahoji ,kuna uhusiano gani kati ya Kikwete na Kennedy au Clinton? Kwanini walinganishwe kwenye makala hii?

Ndugu mwananchi: ukweli ni kwamba hatujui kama Kikiwete atafikia kiwango chao cha ubora au la.Lakini tunalojua ni kwamba Kennedey na Clinton walikuwa miongoni mwa marais vijana waliowahi kuiongoza Marekani,kama itakavyokuwa kwa Kikwete endapo kama atapata ridhaa toka kwa wananchi kuliongoza taifa la Tanzania mwaka huu.

Ni mpaka hapo atakapopewa jahazi na kupewa muda wa kuliongoza ndipo tutajua kwamba anafikia kiwango hicho au la.

Inawezekana kabisa kijana Kikwete akailetea Tanzania mabadiliko makubwa sana ya kiuchumi na kijamii kama Kennedy na Clinton walivyoiletea Marekani,ama yawezekana pia kikwete akaboronga mno kuliko hata wengi tunavyotizamia.

Kwa nchi maskini kama Tanzania,ujana wa Kikwete na uzuri wake hivyo tu havitoshi kabisa kuleta mabadiliko yoyote yale,yawe ya kiuchimi ama kijamii...Kwanini?--kwasababu kama chama tawala kilishindwa kuleta mabadiliko hayo kwa muda wa kipindi chote cha miaka 40 ambayo kimekuwa madarakani,si rahisi kikayatekeleza hayo kwa ndani ya kipindi cha miaka mitano tu.

Mathalani,chukulia swala la ajira kwa vijana.Kwa muda wa miaka arobaini madarakani-CCM ilishindwa kabisa kutatua tatizo hilo.Kikwete ana miujiza gani ya kushusha kazi hizo toka huko zilikojichimbia..?

Tatizo sio suala la ujana,bali tatizo ni ukosekanaji wa sera makini ndani ya chama cha CCM kuhusu mikakati madhubuti ya jinsi ya kutatua tatizo sugu la ajira kwa vijana nchini Tanzania. Mpaka hapo chama kitakapokuwa kimeamua kuketi chini na kuandaa sera zinazoeleweka kuhusu mambo ya ajira hususani-ajira kwa vijana,tatizo hilo bado litazidi kuwepo hata kama angepatikana rais kijana kama alivyokuwa hayati Thomas Sankara wa Burkina Fasso.

CCM wanapaswa kuachana kabisa na wimbo wa "kikwete ni kijana" na badala yake waketi chini na kuandaa sera makini ya jinsi ya kutatua matatizo yanayolikabili taifa likiwemo tatizo sugu la ajira kwa vijana.Kwani kama kigezo ni ujana,basi mgombea wa CUF Prof.Ibrahim Lipumba ndiye anayestahili kuchaguliwa kuwa rais mwaka huu maana yeye ni kijana zaidi ya Kikwete kwani ana miaka 53 tu ukilinganisha na Kikwete mwenye miaka 55.

Hata hivyo,utafiti unazidi kuonyesha kuwa maraisi vijana wanafanya vizuri zaidi kuliko wazee. Kwa hiyo labda ni nafasi yetu sasa [Tanzania] kuwa na raisi kijana, na kama tukimpatia nafasi na ushirikiano anaweza akafanya maajabu kama marais wenzake vijana wa nchi za magharibi kama--Kennedy na Clinton.

Kitu kikubwa tu na cha muhimu sana kwa Bwana Kikwete,ama yeyote yule atakayekuwa amechaguliwa, ni kutafuta watu wenye hekima na ujuzi wa mambo ya utawala ambao watamshauri vyema na kumpa ushauri sahihi.

Na hii ndiyo tofauti kubwa iliyopo kati ya maraisi vijana na wale wasio vijana, kwamba vijana sikuzote wanasikiliza mashauri wapewayo na wanayafanyia kazi nzuri mashauri hayo. Wazee wanadhani wanazo hekima za kutosha tayari na hawahitaji mashauri ya wengine.

Hili tumelishuhudia kwa majirani zetu kama Kenya [chini ya utawala wa Moi],Zimbabwe [Robert Mugabe],na mlolongo unaendelea...

Kwa hiyo ingawa wengine wetu labda hatukufurahia uteuzi wa Bwana Kikwete kuwa mgombea wa CCM, hivyo kumpatia tiketi ya moja kwa moja Ikulu, hakuna tunaloweza kufanya sasa kuzuia hilo kutokea.Labda wapinzani waungane na kumsimamisha mtu tofauti na Mrema,Lipumba,Cheyo,ama Marando.

Na kwa sababu upinzani tanzania bado unalegalega,inaelekea tupende tusipende tutakuwa na kipindi cha miaka mitano au kumi ya utawala wa Jakaya. Ni vyema tujifunze mapema kumpatia nafasi ya kutuonyesha uwezo wake wa uongozi kwa kumpatia ushirikiano--maana mwisho wa siku, kwamba anafanya vizuri au vibaya, ni maisha yetu na wale tunaowapenda ndiyo yanayoathiriwa na mwenendo wa kila siku wa utawala wa serikali.

Mungu Ibariki Tanzania,

.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.