Mh. KIKWETE USITUANGUSHE

Na, Mwandishi wetu

Kama kuna watu ambao wamewahi kuwa na bahati ni mgombea wa CCM bwana Jakaya Mrisho Kikwete. Kama wengine mnavyofahamu, kadri siku zinavyozidi kukaribia kwa yeye kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mambo yanazidi kumnyookea katika maandalizi ya kuchukua hatamu za uongozi.

Hivi karibuni chini ya Uongozi wa waziri mkuu na waziri wa fedha wa Uingereza, nchi tajiri duniani la kundi la G8 zimekubali kusamehe madeni ya nchi maskini 18 Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizofaidika na msaada huo.

Ingawa rais wa Marekani alikataa  wazo zima la mawaziri hao wa uingereza, ila waziri mkuu wa Uingereza ameahidi kuendelea kusukuma ajenda yake, si tu ya kusamehe madeni ya nchi maskini, bali pia kuongeza kiwango cha misaada nchi tajiri zinazotoa kwa nchi maskini.

Vigezo vilivyotumiwa hasa kupata nchi zinazosamehewa madeni ni sera za serikali hizo katika mambo ya utawala bora, kupinga rushwa na uwakili mzuri wa fedha wa serikali na watu wake. Kwa hiyo hiyo ni dalili njema kwa serikali ya Raisi Mkapa kwamba wamefanya vizuri katika hizo nyanja.

Sasa tukirudi kwa bwana Kikwete, ukweli ni kwamba ingawa anaonekana kuwa na munkari mkubwa wa kazi, lakini hadi sasa hakuna anayejua kwamba uwezo wake kiutawala na mipango yake ya maendeleo itakuwaje. Ingawa kwa kiwango kikubwa anakwenda ikulu kuendeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, hilo peke yake halimhakikishii mafanikio.

Ila mpaka sasa lazima tukubali kwamba karibu kila kitu kinafanya kazi upande wake. Inasemekana kwamba tangu uhuru na baada ya uchumi wa nchi kuanza kuyumba, nchi ilikuwa inategemea misaada ya kigeni na mikopo katika bajeti ya serikali na mipango mingine ya maendeleo. Lakini kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania baada ya miaka michache ya Raisi Mkapa kushika hatamu za uongozi, nchi ikaweza kuwianisha bejeti ya serikali bila mikopo na misaada toka nje. Na tangu hapo wameendelea kujitahidi, si tu kuwianisha bajeti, bali pia na kujitahidi kulipa deni la ndani na nje ya nchi, na mara moja moja kutoa misaada kwa nchi za nje kama ambavyo ilitoa tani 3000 za nafaka msaada kwa serikali ya Zimbabwe.

Kwa hiyo sasa ukiangalia manufaa aliyonayo Kikwete kabla hajaingia Ikulu unaona kabisa kwamba kama akiharibu basi atakuwa kiongozi mbovu kuliko wote waliowahi kuwepo.

Kwanza atakuwa anachukua madaraka ya nchi ambayo bajeti yake ya serikali imewiana nasiyo tu kuwiana bali kuna ziada kidogo. Pili hiyo ziada ambayo walikuwa wanaitumia kulipa madeni huko nje sasa itabakia ndani kwa mipango ya maendeleo ikiwa na maana kwamba kama kweli ana mpango mahsusi wa maendeleo ya nchi na wananchi tayari anao mtaji wa kuanzia. Si hivyo tu, bali pia anapokea nchi ambayo tayari iko kwenye muelekeo mzuri sana kimaendeleo na hata hadhi ya nchi katika duru za kimataifa inaanza kukua.

Wakati huo huo mabadiliko ya nguvu ya fedha yetu nayo yameimarika zaidi. wachumi kadhaa wanakadiria kuwa kiwango cha ubadilikaji wa fedha kimeshuka kufikia tarakimu moja kitu ambacho ni kizuri sana kwa kuweka mikakati ya kuongeza nguvu na thamani ya fedha yetu. Lakini zaidi ya yote anakuwa anachukua madaraka ya nchi ambayo haina deni kabisa la nje, kitu ambacho ni kikubwa sana kwa maendeleo ya nchi. Unakuwa ni mwanzo mpya kabisa kwa nchi nzima, utawala mpya, uongozi mpya,uchumi mpya hamna madeni watu wanaanza upya.

Ukiwa na mambo yote haya kukusaidia kuanza utawala wako, huhitaji kufanya maajabu sana kuleta maendeleo, hiyo haina maana kwamba yeye alegelege, anatakiwa bado kufanya juhudi kutusukuma mbele maana mwenzake aliyemtangulia alifanya kazi ya ajabu sana kumuandalia mazingira haya mazuri ambayo yeye ataanzia kazi.

Hivyo kwa wote wale tulio makada wa chama na wale tulio wakereketwa na wafurukutwa wa upinzani, hata kama wale tunaotamani wachaguliwe hawatachaguliwa, nadhani litakuwa jambo la busara kushirikiana na serikali yoyote itakayowekwa ili kuendeleza mwenendo wa maendeleo ambayo nchi yetu imeshafikia na inaendelea kufikia.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.